Na. Shahanazi Subeti, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri aliitaka jamii kuzingatia suala la usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kujikinga na magonjwa na kufanya mji kuwa safi na salama katika kipindi hiki cha maandalizi ya bajeti ya halmashauri ili wananchi wawe na afya bora.
Aliyasema hayo katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Dodoma kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya kupokea na kujadili mapendekezo ya rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa fedha 2025/2026.
Alhaji Shekimweri alisema “wenzetu maafisa afya, watendaji wa kata, changamoto za uchafu wa mji wetu ni usimamizi kwa sehemu fulani, yapo maeneo ya kampuni za usafi, yapo maeneo yanavikundi vya usafi, lakini ni wajibu wa mwananchi mmoja mmoja kufanya usafi wa eneo lake. Kwahiyo, tuimarishe usimamizi, na kuna makampuni na vikundi na vinalipwa kwa kufanya kazi hizo”.
Akiongelea suala la usalama katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa kamera za usalama (CCTV) ni muhimu katika kuimarisha usalama. “Tunachokimaanisha tunapoelekea utaona askari wachache barabarani wanapita kwenye doria, kwasababu kutakuwa na Kamera zinazofanya kazi, badala ya kutuma askari, watakuwa wanaona tukio, lakini katika baadhi ya maeneo ya “observation points” watakaa na pikipiki zao ili kukamata watu wanaofanya matukio ya wizi. Tunataka tuelekee katika mazingira ambayo hakuna ‘panyaroad’ Dodoma, kwasababu muda wote mji unaangaliwa na mitambo ya kisasa kupitia Jeshi la Polisi na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama” alisema Alhaj Shekimweri.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma alisema kuwa amepokea mchango unaohusu mkakati wa dharura na majanga. “Mfano jana kulikuwa na tukio la moto, wengi mmeona fremu takribani 12 na stoo mbili ziliungua kwa moto lakini tukabaini Jiji letu lina 'fire hydrant’ (mitambo ya kuunganisha kwa ajili ya kuzimia moto) 74 mji mzima, lakini ambazo zinafanya kazi hazizidi 40. Kwahiyo, Jiji limepokea hiyo rai kwa haraka kulisaidia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwasababu wananchi ni wa halmashauri. Hivyo, ni wa kamati hii ya ushauri wa maendeleo ya wilaya na ndio walipa kodi. Kwahiyo, ni jambo la wananchi wetu tufanye huduma ya mitambo hiyo” alisema Alhaj Shekimweri.
Aliwataarifu wajumbe kuwa bajeti ya halmashauri inategemea ukusanyaji wa kodi na kuwataka kudai risiti kwa kila malipo wanayofanya. “Ndugu zangu wafanyabiashara, wanataka kuongeza faida, anaweza kukuuzia na asikupatie
risiti yeye atapata faida lakini wewe utakuwa umeidhulumu serikali na umejidhulumu wewe mwenyewe. Maendeleo yote haya hayawezi kufanyika kama haukusanyi kodi” alisema Alhaj Shekimweri.
Nae, Katibu wa AAFP, Zuhura Mganga, aliishauri serikali kuhusu Soko la wazi la Machinga kufungwe CCTV kamera za kutosha ili kuzuia vitendo vya wizi. “Nashauri kuhusu usalama wa Soko la wazi la Machinga pale kumekuwa na wizi, hakuna kamera za kutosha na hata kamera zilizopo hazioneshi pande zote” alisema Mganga.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu Bakwata, Kakongwe Misambano, alichangia katika suala la afya na usalama barabarani. “Kwa upande wa afya, ukiangalia tunaongelea bajeti sana lakini utendaji wake unakuwa hauko sahihi. Mfano, mitaro ya barabara ya Nkuhungu ambayo imetengenezwa kwa ajili ya bwawa, na linahamisha watu kila mwaka wakati wa mvua, usalama kwa watoto hakuna kwasababau maji hayaendi badala yake yanatuwama. Kwahiyo, …bajeti ambazo zinatengwa zinafanya nini?. Kwasababu, hiyo mitaro inarudisha nyuma, badala ya kupeleka mbele ili maji yaishe” alisema Misambano
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.