Na Binde Constantine, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ametoa rai kwa wadau wa elimu kuendelea kujitokeza kusaidia sekta ya elimu kwani bado kuna uhitaji wa vifaa vya kujifunzia kutokana na ongezeka la uandikishwaji wa wanafunzi.
Aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya upokeaji wa madawati kwa ajili ya shule ya sekondari Mbabala kama msaada kutoka Benki ya Stanbic iliyofanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo Septemba 22, 2021.
“Kumekua na ongezeko kubwa sana la uandikishaji wa wanafunzi, kufuatia utekelezaji wa waraka wa elimu bila malipo, waraka wa elimu namba tano na namba sita, wazazi wameitumia fursa hiyo vizuri na matokeo yake miundombinu imekua haikidhi mahitaji” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sospeter Mazengo alisema, Halmashauri ya Jiji inapambana katika kuhakikisha wanaondokana na changamoto ya upungufu wa madawati katika shule zote za jiji hilo.
“Sisi kwa upande wetu kama Halmashauri tunapambana na changamoto ya kutatua upungufu wa madawati katika shule zetu lakini tunapoona taasisi binafsi kama Benki ya Stanbic wanaliona hili na kuamua kutuunga mkono basi tunafarijika sana, kwa hiyo tunawashukuru na kuwakaribisha tena Dodoma” alisema Mazengo.
Naye diwani wa Kata ya Mbabala Paskazia Mayala aliomba ushirikiano baina ya Serikali na taasisi binafsi katika kuhakikisha shule zote za Jiji la Dodoma zinaondokana na adha ya upungufu wa madawati “sisi tunaomba ushirikiano baina ya serikali na taasisi binafsi ziweze kutuunga mkono katika kuhakikisha watoto wetu wanasoma kwenye mazingira mazuri” alisema Mayala.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.