MKUU wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amekabidhi tuzo na zawadi kwa washindi wa uchoraji wa alama za barabarani kwa wanafunzi wa shule za msingi huku akibainisha kuwa Dodoma kama makao makuu wanahakikisha miradi yote ya barabara inakuwa na miondombinu yote ya usalama wa barabarani kuepukana na ajali za mara kwa mara.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadi hizo katika shindano linazoendeshwa na Kampuni ya Puma Energy na Shirika la Amend, Shekimweri amesema ameguswa na mafunzo hayo kwani yatasaidia kuokoa maisha ya watoto na kupitia mashindano hayo wanajenga uwezo kwa watoto tangu mtotoni kuzitambua alama za barabarani.
Ameongeza kuwa “Takwimu za watu wanaopata ajali za barabarani bado ni kubwa, nafikiri kuna haja ya kuongeza elimu ili kupunguza au kuondoa kabisa vifo vya watoto, wazee na wenye ulemavu nawataka Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani jijini Dodoma kuongeza mafunzo kwa wanafunzi ambao wamekua wakisimama barabarani kuzuia magari ili wanafunzi kuvuka sambamba na kuwapatia vifaa.
“Tutaendelea kusimamia sheria ya usalama barabarani, nitoe rai kwa Jeshi la Polisi kuwa wakali kwa wanaovunja sheria za barabarani, haiwezekani mtu anatembea mwendo kasi sehemu ambayo kibao kinamuonesha kutembea mwendo mdogo” amesema, Shekimweri.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa Puma, Godluck Shirima akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Puma, Dominic Dhanah ameishukuru Serikali kwa namna ambavyo wametoa ushirikiano kwao wakati wa utekelezaji wa mafunzo hayo huku akiahidi kuwa wataendelea kutoa mafunzo hayo kwa wanafunzi lengo likiwa ni kutokomeza kabisa ajali za barabarani.
Amesema utoaji wa zawadi hizo unahitimisha mradi uliotekelezwa na Puma na Amend ambao ulihusisha mafunzo kuhusu usalama barabarani na uchoraji wa picha kwa shule za Kisasa, Ipagala B, Chidachi, Makole na Dodoma Mlimani ambapo wanafunzi wasiopungua 20,000 walipata mafunzo hayo.
“Huu mpango huu wa usalama barabarani ni mwendelezo wa kampeni ambayo ilizinduliwa rasmi miaka tisa iliyopita ambapo zaidi ya shule 100 zimefikiwa na wanafunzi zaidi ya 120,000 mikoa mbalimbali wamepata mafunzo hayo,” alisema.
Amesema kwa njia hiyo Puma Energy inaamini kuwa watoto watakuwa salama na kutakuwa na taifa lenye watu imara na wenye nguvu za kulitumikia taifa lao.
”Lengo letu kama kampuni ni kuongeza wigo ili kufikia shule nyingi zaidi nchi nzima kwa mwaka 2022, sisi kampuni ya Puma Energy tunaahidi kuendelea kuwekeza katika kampeni ya usalama barabarani kwa kushirikiana na serikali kupitia jeshi la Polisi ili kuokoa maisha ya watanzania,” Amesema Shirima.
Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Polisi ambaye amemwakilisha Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma Leonce Kaimukirwa amesema wamefurahishwa na mafunzo ambayo yamekuwa yakitolewa na Amend kwa kushirikina na Kampuni ya Puma Energy Tanzania na kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likitoa mafunzo ya usalama barabarani.
“Tumekuwa tukitoa elimu katika shule za msingi, shule za sekondari ,vyuoni pamoja na watumiaji vyombo vya moto wakiwemo waendesha bodaboda, tumekuwa tukielimisha wazazi kutopakia watoto wao kwenye bodaboda, tunawashauri wazazi wasikubali watoto kubebeshwa zaidi katika bodaboda,” amesema.
Nae Meneja Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la Amend Tanzania Simon Kalolo ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo amesema wamekuwa wakitekeleza miradi mingi katika nchi zaidi ya 10 barani Afrika ikiwemo Tanzania lengo ni kutoa elimu ya usalama barabarani kuondoa au kupunguza ajali za barabarani.
Katika shindano hilo mwanafunzi Joseph Thadei kutoka shule ya Msingi Chidachi aliibuka mshindi na kuzawadiwa shilingi laki tano na nafasi ya pili kuchukuliwa na Emmy Martin aliyezawadiwa laki tatu na nafasi ya tatu kuchukuliwa na Emanuel Umega aliyezawadiwa laki mbili wote wawili kutoka shule ya msingi Kisasa huku shule ya msingi Chidachi ikizawadiwa kiasi cha shilingi milioni nne na kikombe cha ushindi kwa kuibua mshindi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.