Na Noelina Kimolo
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabar Shekimweri amewataka wazazi wote wilayani humo kutambua na kuthamini umuhimu wa walimu ambao wanamchango mkubwa katika kuleta matokeo mazuri kwa wanafunzi pamoja na kuwapunguzia wanafunzi hao majukumu ya nyumbani ili wapate muda zaidi wa kujishughulisha na masomo.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza kupitia mahojiano yaliyofanyika katika kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na kituo cha runinga cha Star cha Jijini Mwanza.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, wazazi ni muhimu kushirikiana katika kuleta matokeo mazuri kwa wanafunzi pamoja na kuwatia hamasa kwa kufuatilia maendeleo yao kitaaluma kwa kipindi chote watakachokuwa masomoni.
“Ni vyema tushirikiane na walimu, wazazi, pamoja na bodi ya shule ili kuleta maendeleo na kujenga hamasa ya watoto kusoma, pia ni muhimu tuwe na maandalizi kabambe ya mitihani ya taifa” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha, Shekimweri aliahidi kusimamia vyema kilimo cha zao la zabibu katika kipindi chote cha uongozi wake ili kuinua uchumi wa wakazi wa Wilaya hiyo na kuimarisha ajira kupitia zao la zabibu linalolimwa zaidi katika Mkoa wa Dodoma.
‘’Ni lazima tukuze uchumi wetu na wananchi wa Wilaya hii wawe sehemu ya uchumi unaokua, vijana wapate ajira ili kupunguza matukio ya uharifu kama vile wizi na udokozi, naamini tukiweka nguvu na kuhamasisha hakika tutakuwa na maendeleo” alisema Shekimweri.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.