Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kuanzisha Kliniki ya Ardhi iliyowafanya wataalam kutoka ofisini na kuweka kambi kuwahudumia wananchi eneo moja ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo eneo la Manispaa ya zamani alipotembelea na kukagua maendeleo ya Kliniki ya Ardhi inayotoa huduma jijini hapa.
Shekimweri alisema “kipekee nimpongeze Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, niliyasema haya wakati tunakupokea hapa Dodoma baada ya kuteuliwa. Mimi nakufahamu unavyofanya kazi. Ninafahamu ni mtu unaejali sana watu na matatizo ya wananchi. Nilikuwa nawaambia wananchi ninajua kuna mkurugenzi atawasilikiza kwa nafasi na kwa staa na atawashughulikia matatizo yenu yaliyowasumbua kwa muda mrefu”.
Alisema kuwa Rais alishaelekeza wataalam kutoka ofisini na kwenda kwa wananchi kutatua kero zao. “Haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba tutoke ofisini na kwenda kushughulikia matatizo ya wananchi. Na hapa Dodoma sekta ya Ardhi ndiyo kero sugu. Tatizo kubwa lazima lishughulikiwe kwa ukubwa wake. Nimekuja hapa kukupongeza na kukutia nguvu pamoja na menejimenti, lakini kupongeza utaratibu huu. Hapa wataalam wote wapo hivyo hakuna kupigana tarehe” alisema Shekimweri.
Mkuu huyo wa wilaya aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika kliniki hiyo. “Niwapongeze wananchi wote mliojitokeza kwa wingi siku ya leo. Jana wananchi zaidi ya 1,000 walijitokeza hii inaonesha mlivyo na imani na serikali yenu katika kutatua kero zenu. Niwaombe kuendelea kutuamini tuna dhamira ya dhati kushughulikia matatizo yenu” alisema Shekimweri.
Akiwa katika kliniki hiyo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma pamoja na mambo mengine alikabidhi hati miliki saba kwa wananchi zilizoandaliwa muda mfupi uliopita.
Kwa upande wake mwananchi wa Dodoma mjini, Mwajuma Seja alimshukuru Mungu kwa kupata hati yake. “Mheshimiwa Mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa jiji pia nawashukuru sana kupata hati yangu. Sipo peke yangu wapo wenzengu 24, mimi peke yangu ndio nimebahatika kupata Hati wenzangu wote hawajapata hata ‘control number’ alisema Seja kwa masikitiko.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.