Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WILAYA ya Dodoma imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha shilingi 580,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 29 ya shule za sekondari ili kuwawezesha wanafunzi wa kidato cha kwanza kusoma katika mazingira bora na salama.
Shukrani hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokabidhiwa madarasa 29, ofisi 24 na viti na meza 1,450 katika shule ya sekondari Ng’hoghona iliyopo jijini Dodoma.
Shekimweri alisema “tunamshukuru sana Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwanza siyo tu kwa fedha alizozitoa lakini kwa kufikiria kizalendo namna sahihi ya matumizi ya fedha za Uviko-19 na kuweka tofauti na viongozi wengine karibia wote wa Afrika. Fedha za Uviko -19 zimetolewa na Benki ya Dunia kama mchango wao kwenye mapambano ya Uviko-19. Maono ya Rais wetu na dhamira njema siyo tu kuwa na matumizi ya mara moja lakini uendelevu wa kushughulika na changamoto. Alijihoji na kutusaidia kutupatia dira kushughulika na jambo hili. Ikiwa Uviko-19 inatokana na msongamano kumbe namna ya kushughulika na Uviko-19 pamoja na kunawa maji ni kuondoa msongamano”.
Mkuu huyo wa wilaya aliridhishwa na matumizi ya fedha na kusema kuwa fedha hiyo imetumika kwa maeneo yaliyokusudiwa na kuona fahari kwa kazi iliyofanyika. “Namna ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, namna ya kumtia nguvu na namna ya kuomba maeneo mengine atuangalie pamoja na kushukuru kwa kiwango cha juu cha kushukuru. Sisi tunashukuru sana ametusaidia parefu sana tumesikia taarifa ya Mkurugenzi wa Jiji kuwa maoteo yetu ni kusajili watoto 12,151” alisema Shekimweri.
Akitoa taarifa ya makabidhiano ya madarasa 29, ofisi 24 na meza na viti 1,450 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatarajia kupokea wanafunzi 12,151 watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023. “Idadi hii ya wanafunzi ni nyongeza ya wanafunzi 3,140 ukilinganisha na wanafunzi waliojiunga kidato cha kwanza mwaka 2022. Kufuatia upungufu uliokuwepo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipokea kiasi cha shilingi 580,000,000 katika shule 23 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 29” alisema Mafuru.
Alisema kuwa halmashauri yake ilitekeleza mradi huo kwa njia ya “force account” ambapo wakuu wa shule walikasimishwa madaraka ya usimamizi wa mradi huo. “Mradi ulianza tarehe 10 Oktoba, 2022 kwa shule zote 23 na usimamizi na ufuatiliaji ulifanywa na ofisi ya Mhandisi wa Jiji na wataalam wengine pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Dodoma na wadaun wengine. Kufukia tarehe 30 Novemba, 2022 ujenzi huo ulikamilika kwa shule zote 23 ambapo madarasa 29 yalijengwa, ofisi za walimu 24 pamoja na meza na viti 1,450 kwa wastani wa meza na viti 50 kwa kila darasa” alisema Mafuru.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.