Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepongezwa kwa kuandaa vizuri Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa kuzingatia miongozo na vipaumbele vilivyowekwa ikitajwa kuwa itakwenda kujibu changamoto katika jamii.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea katika kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Dodoma cha kupitia mapitio ya bajeti ya mwaka 2021/ 2022 pamoja na mpango wa makisio ya mapato na matumizi ya mwaka 2022/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauiri hiyo leo.
Shekimweri alipongeza miongozo mbalimbali na vipaumbele vilivyowekwa na Jiji la Dodoma katika Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023. Aidha, alipongeza andiko la Mpango na Bajeti ya halmashauri chini ya Mkurugenzi na timu yake ya menejimenti na kulitaja kuwa ni andiko zuri linalojitosheleza kujibu changamoto za wananchi wa Jiji la Dodoma.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akitoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuongeza kuwa fedha zote zinafika kwa wakati. Alisema kuwa Jiji la Dodoma limekuwa kilifanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Alisema kwa fedha shilingi bilioni 2.940 zilizotolewa katika fedha za mapambano dhidi ya UVIKO-19, madarasa yote 147 pamoja na samani zake yamekamilika. Alisisitiza kuwa changamoto iliyopo ni ya uwiano wa madarasa, wanafunzi na matundu ya vyoo, na kushauri bajeti hiyo iongeze ujenzi wa matundu ya vyoo kwa shule katika jiji hilo.
Aidha, alishauri halmashauri ianze kuainisha maeneo yenye uhitaji wa madarasa mengine na kujipanga kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya ghorofa. Alisema kuwa sababu kubwa ni maeneo yaliyopo ni yaleyale hayaongezeki.
Akiongelea Mpango na Bajeti wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Mchumi wa Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alisema kuwa Mpango na Bajeti umezingatia vipaumbele mbalimbali. Alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imejipanga kuelekeza nguvu zake katika kuweka mazingira wezeshi yatakayosababisha kuinua na kukuza uchumi wa halmashauri na kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja kwa kuwekeza katika miundombinu ya uchumi na kutoa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. “Fedha zitakazotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, asilimia 60 ya kiasi hicho kitaelekezwa kwenye miradi yenye tija itakayozalisha ajira. Kufungua akaunti kwa ajili ya marejesho ya asilimia 10 ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Pia marejesho hayo ya mikopo ya asilimia 10 yanayotarajiwa kurejeshwa na vikundi vilivyokopeshwa yataingizwa kwenye Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023” alisema Kaunda.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.