Na Sifa Stanley na Binde Constantine, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara katika Mji wa Serikali Mtumba zinazojengwa na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Dodoma.
Mkuu huyo wa Wilaya alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara unaoendelea katika mji wa serikali na kusimamiwa na TARURA Wilaya ya Dodoma.
Shekimweri alisema kuwa ameridhishwa na ujenzi wa barabara unaoendelea katika mji wa serikali. Aliagiza kukamilisha mradi huo ifikapo tarehe 31 Disemba, 2021 kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba ili barabara hizo zianze kutumika. “Mmetoa sababu za kuchelewesha mradi, tumewaongeza miezi mitano. Miezi mitano ni mingi, simamieni mradi ili ukamilike kwa muda uliopangwa” alisema Shekimweri.
Aidha, aliagiza suala la upandaji miti katika barabara hizo ili kuendelea kutunza mazingira. Alisema kuwa upandaji miti ni utekelezaji wa ajenda ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kupanda miti na kuifanya Dodoma kuwa ya kijani. “Tutekeleze ajenda ya Makamu wa Rais ya kupanda miti kwa kuhakikisha tunapanda miti, mradi unapoendelea wadau wakijitokeza hasa wa mazingira tuwape nafasi ya kupanda miti” aliongeza Shekimweri.
Naye Mkurugenzi wa Barabara za Mijini kutoka TARURA, Mhandisi Mohamed Mkwata akizungumzia maendeleo ya mradi huo, alimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa mradi utakamilika kwa wakati. Alisema kuwa Mkandarasi ameongeza juhudi katika utekelezaji wa mradi ili ukamilike kwa wakati. “Mkandarasi ameongeza mitambo na vifaa vya ujenzi ikiwemo mitambo ya kusaga kokoto na mitambo ya kuzalisha lami. Pia anafanya kazi siku zote za wiki ili kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati” alisema Mhandisi Mkwata.
Mkuu wa Wilaya alifanya ziara katika maeneo makuu mawili ya mradi huo ambayo ni eneo la kusini na eneo la kaskazini, eneo la kusini la mradi huo limetengwa mahususi kwa ujenzi wa ofisi za wizara za Serikali na mabalozi, eneo la kaskazini limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za ubalozi wa Marekani na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.