Na. Theresia Francis, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ameridhishwa na kupongeza hatua ya ujenzi wa mradi wa shule ya sekondari Hombolo Makulu unaoendelea kujengwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa gharama ya shilingi milioni 470.
Alitoa pongezi hizo katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Dodoma, alipotembelea ujenzi wa sekondari hiyo katika Kata ya Hombolo Makulu jijini hapa jana.
Mkuu huyo wa wilaya baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa shule hiyo, alisema kuwa ameridhishwa na hatua ya ujenzi unaoendelea. Alisema kuwa mradi huo una akisi fedha iliyotolewa na serikali kuu chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Shekimweri alishtushwa kuona ndani ya mradi huo kuna nyumba binafsi imejengwa na kusema kuwa kitendo hicho kinahatarisha usalama wa wanafunzi na wafanyakazi katika mradi huo. Alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya kumchukulia hatua mmiliki wa nyumba hiyo. "Nilitoa maelekezo mara ya mwisho kuhusu nyumba ile iliyopo ndani ya mradi wa shule naona hamkulifanyia kazi. Sasa OCD mchukulie hatua mmiliki wa nyumba hiyo" alisema Shekimweri kwa ukali.
Kwa upande wake Afisa elimu ya sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alitoa shukrani kwa Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa mradi huo wa shule ya sekondari. Alisema kuwa shule hiyo ina jumla ya madarasa nane, Maabara tatu, jengo la Maktaba, jengo la TEHAMA pamoja na matundu 20 ya vyoo.
“Shule hii ni mkombozi katika kata yetu, wanafunzi wamekua wakitembea umbali mrefu zaidi ya kilomita tisa kufuata huduma ya elimu. Hivyo, basi shule hii itasaidia kwa kiasi kikubwa watoto wetu hususani watoto wa kike" alisema Mwalimu Rweyemamu.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma aliambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya, Afisa elimu ya sekondari wa Jiji la Dodoma, Diwani wa Kata ya Hombolo Makulu pamoja na maafisa waandamizi wa serikali.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri (wa tatu kutoka kulia) alipotembelea kuona maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Hombolo Makulu akiambatana na Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma Mwalimu Upendo Rweyemamu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.