Na Sifa Stanley, Dodoma
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ameiagiza Halmashauri ya Jiji na wadau mbalimbali wa utunzaji wa mazingira Jijini Dodoma kuhakikisha mazingira ya Jiji hilo yanafanyiwa usafi, na kuwa safi muda wote na kutunzwa.
Shekimweri alisema hayo wakati wa kikao kazi cha wadau wa mazingira kilichofanyika katika ukumbi wa Polisi jamii Agosti 26, 2021 kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuainisha changamoto mbalimbali za kimazingira Jijini humo.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa ni wajibu wa viongozi kusimamia suala la usafi wa mazingira, pia wadau wa mazingira lazima wawajibike katika utunzaji wa mazingira ili kuliweka Jiji la Dodoma katika hali ya usafi.
“Sisi ni jiji la sita, sisi ni Makao Makuu, tumejengewa soko kuu kubwa, uwanja mzuri wa ndege unajengwa, na stendi nzuri, kwa uwekezaji huu wote tuliofanyiwa na Serikali hivi kweli tuchafue mazingira?, tuhakikishe tunatunza mazingira ili iwe kama njia ya kuishukuru Serikali ya awamu ya tano na sita kwa maendeleo waliyotufanyia”alisema Shekimweri.
Naye Mkuu Wa Idara ya Mazingira na Udhiti Taka Ngumu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alieleza namna idara hiyo inavyofanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha mazingira ya Jiji yanatunzwa, na usafi katika Jiji unaimarika ikiwemo suala la kufanya usafi kila Jumamosi ili kuhakikisha jiji linaendelea kuwa safi wakati wote.
“Tunaendelea kuhimiza utunzaji wa mazingira, na zoezi la usafi kila jumamosi ni endelevu ambapo Jumamosi hii tutakuwepo Kata ya Kilimani kwa ajili ya kuungana na wakazi wa Kata hiyo kuhamasisha na kufanya usafi pamoja” alisema Kimaro.
Akisisitiza suala la kutunza mazingira, Afisa Mazingira na Udhibiti Taka Ngumu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ally Mfinanga aliwataka wadau hao wa mazingira kutumia njia sahihi za utunzaji taka na kuepuka uchomaji na ufukiaji wa taka ili kuepusha uchafuzi wa mazingira huku akiwakumbusha kuendeleza tabia ya upandaji miti ili kuendelea kuweka mazingira katika hali ya usafi na usalama.
“Kwa wakazi wote wa Tarafa ya Dodoma Mjini, ni marufuku kuchimba mashimo ya taka na kuchoma taka, vitendo hivyo vinachangia kuchafua mazingira” alisema Mfinanga.
Wadau wa mazingira walioshiriki kikao kazi hicho ni pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini Tanzania (TARURA), Wakala wa Barabara (TANROADS), Makampuni yanayojishughulisha na kazi za usafi, wadau wa erejelezaji wa taka, na watendaji mbalimbali wa ngazi ya Kata.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.