Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WILAYA ya Dodoma ipo katika mapambano makubwa ya UVIKO-19 ikihakikisha elimu sahihi inatolewa kwa wananchi na kutekeleza maelekezo ya serikali kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri (wa kwanza kulia pichani juu) alipokuwa akiongea na wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo.
Shekimweri alisema kuwa dunia ipo kwenye mapambano dhidi ya UVIKO-19, na Wilaya ya Dodoma haipo kisiwani. “Tunaendelea kupeana elimu ya kujikinga na ugonjwa huu na kukumbushana maelekezo ya serikali. Kwa takwimu za leo, Duniani vimetokea vifo takribani milioni 4 vya ugonjwa wa UVIKO-19. Hii ni vita kubwa. Tufike mahali tukubali kuwa elimu imetosha na tutekeleze maelekezo ya serikali ili watu wetu wasife” alisema Shekimweri.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alisema kuwa ugonjwa wa UVIKO-19 unaambukizwa kutoka kwa mtu au watu kwa kushikana na majimaji toka kwa mtu aliyeambukizwa kwenda kwa mwingine. “Ili kujikinga, ni muhimu kuchukua hatua kwa kuvaa barakoa, kunawa kwa maji tiririka na sabuni na kutumia vitakasa mikono” alisema Dkt. Method.
“Ukipata chanjo unaujengea mwili uwezo wa kupambana na UVIKO-19. Ukipata chanjo unapunguza uwezekano wa kuambukizwa. Hata unapoambukizwa hali haiwi mbaya sana kama ambaye hajachanja. Uzoefu unaonesha kuwa maeneo ambayo watu wengi wamechanja, idadi ya maambukizi inashuka na vifo vimepungua sana. Chanjo hizi ni salama. Mimi mwenyewe nimechanja na leo naendelea na kazi kama kawaida” alisema Dkt. Method.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.