Na. Jackline Patrick na John Masanja, DODOMA
MASHIRIKA yasiyo ya Kiserikali yametakiwa kuzitazama changamoto mbalimbali katika jamii na kuzitumia kama fursa kwa utoaji wa elimu na kuisaidia jamii kuondokana nazo.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki katika Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Dodoma. Jukwa hilo limefanyika Agosti 27,2024 katika ukumbi wa mikutano, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa (Mkapa House).
Akizungumza wakati wa hotuba yake,Mhe. Shekimweri aliyapongeza Mashirika yasiyo ya Kiserikali katika jitihada zake za kuihudumia jamii kwenye masuala mbalimbali ya kimaisha kupitia huduma wanazozitoa, huku akiwataka kuzidi kuisaidia Serikali.
Aidha, Mhe. Shekimweri aliyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuisaidia Serikali katika kutoa elimu itakayozuia ukatili kwa watoto, unyanyasaji wa kijinsia pamoja matumizi ya dawa za kulevya. Alisema masuala hayo yamekuwa ni changamoto kubwa katika jamii ya sasa.
“Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yafanye kazi kwa uhuru, kwa kuzingatia sheria, kanuni. Kazi ifanyike kwa uzalendo kwa kuzingatia maadili ya Nchi yetu” alisisitiza Shekimweri.
Sambamba na hayo,Shekimweri aliwapongeza wajumbe kwa kuhudhuria katika Jukwaa hilo, na kuwataka kwenda kuyafanyia kazi yote waliyojifunza kwa ustawi na maendeleo ya jamii.
Awali wakati wa ufunguzi, Msajili Msaidizi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Dodoma, Honoratha Rwegasira alisema lengo kuu la jukwaa hilo ni kuimarisha mahusiano baina ya Serikali, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Wadau wengine pamoja na kutambua mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya Nchi.
"Kuna malengo mahususi ambayo ni kuimarisha mahusiano ya Serikali na wadau wengine kwa ajili ya kutambua mchango wa Mashirika Yasio ya Kiserikali ambapo tumekusudia katika Jukwaa hili kujadili namna mashirika haya yanavyoshiriki kutekeleza mipango ya kitaifa".Alisema Rwegasira.
Vilevile aliongezea kwa kusema “Wadau wote waweze kushirikiana, kuleta huduma bora, kuimarisha uchumi ili kumhudumia Mwanachi, kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uratibu na usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, maana kuna mashirika ambayo ni machanga, hivyo watakapokutana na wazoefu wataweza kupata uwelewa mkubwa na kushirikishana katika fursa, changamoto na mafanikio".
Rwegasira alihitimisha kwa kusema kuwa jukwaa hilo ni fursa mojawapo, kwasababu wajumbe wataweza kubadilishana mawazo na kujenga urafiki wa pamoja kwa ajili ya maendeleo na uhusiano mzuri.
Kaulimbiu ya Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Dodoma 2024 ni “Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni Wadau Muhimu, Washirikishwe Kuimarisha Utawala Bora".
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.