Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WAJUMBE wa Kamati ya Ushauri Wilaya ya Dodoma (DCC) wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kushawishi wananchi kulipa kodi na kudhibiti upotevu wa mapato ili halmashauri iweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Ushauri huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alipoongoza kikao hicho maalum kwa ajili ya kujadili rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Shekimweri alisema kuwa bajeti inayotumika ni ‘cash bases’, unapanga vipaumbele na kiasi cha bajeti kinachopangwa kukusanywa. “Ukishapanga ukiambiwa sawa, unakwenda kukusanya kwa ajili ya kutekeleza. Kama hakuna makusanyo utashindwa kwenye utekelezaji. Niwaombe kila mmoja humu ndani aone ni wajibu wake kuhamasisha wananchi kulipa kodi na kudhibiti upotevu wa mapato kwenye wilaya yetu. Kila mjumbe akafanye wajibu wake kuhakikisha mapato yanapatikana” alisema Shekimweri.
Mkuu wa wilaya alishauri kuimarisha mifumo ya kieletroniki ya kukusanya mapato. “Ni vema tukaimarisha maeneo hayo na kuimarisha makusanyo kwenye ‘D centers’ zetu na miundombinu yake ili ziweze kutoa huduma. Masoko yanaamka na wafanyabiashara wadogo wanahamia kule na mapato yanaongezeka na wananchi wanatembea umbali mfupi kupata huduma” alisisitiza Shekimweri.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imekadiria kukusanya na kutumia mapato yenye jumla ya shilingi 128,278,555,369 kutoka vyanzo katika vyanzo vyake vya ndani, serikali kuu, wahisani kwa ajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo, utoaji huduma na kujiendesha.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.