Wakuu wa wilaya mkoani Dodoma wametakiwa kusimamia katazo la serikali la matumizi ya mifuko ya plastiki katika maeneo yao ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Patrobas Katambi katika uzinduzi wa kikosi kazi cha ukaguzi wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki tukio ambalo limefanyika katika eneo la ‘Independent square’ jijini Dodoma leo.
Wakazi wa Jiji la Dodoma walioshiriki uzinduzi wa kikosi kazi cha kusimamia katazo la mifuko ya plastiki wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Patrobas Katambi
Katambi amesema “Dodoma lazima tuwe wa mfano, tusirudi nyuma, tusiwaangushe viongozi wetu. Leo natangaza rasmi kuwa waheshimiwa wakuu wa wilaya wote wa Mkoa wa Dodoma wasimamie katazo la Serikali la matumizi ya mifuko ya plastiki”. Halmashauri ya Jiji la Dodoma, inatakiwa kuwa jiji la mfano katika kumpa heshima Rais Dkt John Magufuli, aliongeza. Aidha, alisema kuwa halmashauri ya jiji la Dodoma itakuwa ya kwanza katika usafi wa mazingira kitaifa mwaka 2019.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kutafuta na kupata uelewa wa taarifa mbalimbali zinazohusu makatazo ya mifuko hiyo ili kuepuka adhabu zilizowekwa. Alionya kuwa, mtu kutojua sheria si kigezo cha kumfanya asiadhibiwe pale ambapo atapatikana na kosa la kuvunja sheria. “Wajibu wa wananchi ni kutafuta taarifa sahihi za makatazo ya mifuko ya lastiki. Zoezi la ukaguzi linapoanza atakayekutwa na mifuko ya plastiki atapigwa faini kwa mujibu wa sheria” alisema Katambi.
Akiongelea kikosi kazi cha ukaguzi, Katambi amesema “Nazindua rasmi kikosi kazi kitakachoenda kukagua mifuko la plastini katika maeneo mbalimbali. Kikosi kazi hiki tupo vizuri, usithubutu kukaidi katazo hili. Akifafanua zaidi Katambi amesema faida kubwa ipo kwetu wananchi tunapoacha matumizi ya mifuko ya plastiki, hivyo ni vizuri mkaamini kuwa viongozi wetu wana maono ya mbali kwa nchi yetu” alisema Katambi.
Viongozi wakishiriki katika kufanya usafi katika mtaa wa 'One way' jiji Dodoma kabla ya uzinduzi rasmi wa kikosi kazi ya katazo la mifuko ya plastiki.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy alisema “leo tunazindua rasmi katazo la mifuko ya plastiki. Ni vizuri wote kuelewa kuwa hili ni zoezi za kudumu, si la mpito”. Aidha, aliongeza kuwa wasafiri wanaopita Dodoma watakaguliwa ili kuwabaini watakaokuwa na mifuko hiyo. Hakutakuwa na masuala ya kisiasa katika utekelezaji wa katazo hilo, aliongeza.
Awali mkuu wa idara ya Mazingira na udhibiti wa taka ngumu wa Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro aliwapongeza wananchi wote waliojitoleza kushiriki katika zoezi la kuzibua mifereji na kuondoa mifuko la plastiki iliyokuwa ikisababisha mifereji hiyo kuziba.
Nae mfanya biashara katika eneo la barabara ya "One way", Shio Patrick alipongeza zoezi la usafi lililofanyika katika eneo hilo na kushauri liwe endelevu. “Changamoto kubwa ya usafi katika eneo hilo ni baadhi ya wenye nyumba kukaidi kutoka kufanya usafi. Naomba serikali iwahamasishe wenye nyumba hao kutoka na kushiriki pamoja na watu wengine kufanya usafi” alisema Patrick.
Wakazi wa Jiji la Dodoma, watumishi wa Jiji na wafanyakazi wa Kampuni ya usafi ya Green Waste wakifanya usafi kwenye mfereji wa 'Pombe River'
Uzinduzi wa kikosi kazi kwa ajili ya ukaguzi wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki ulitanguliwa na zoezi la usafi lililofanyika barabara ya nane na ‘One way’ likiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Maduka Kessy.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.