MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dkt Binilith Mahenge ameishauri Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuongeza vituo vya mapumziko (recreational centers) kwa lengo la kukabiliana na idadi kubwa ya watu jijini.
Kauli hiyo ameitoa jana alipofanya ziara ya kawaida ya kutembelea na kukagua miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Dkt. Mahenge alisema kuwa baada ya kutembelea na kukagua mradi wa uboreshaji wa mandhari ya eneo la kupumzikia (recreational park) katika eneo la Chinangali na kujiridhisha na hali ya ujenzi unaoendelea, ameona uhitaji wa maeneo mengine ya kupumzikia. “Ushauri wangu, kwa kuwa Jiji la Dodoma linakuwa kwa kasi, hatuwezi kuwa na ‘recreation center’ moja. Ni vizuri ziwepo zaidi ya moja. Barabara ya Singida iwepo, barabara ya Arusha iwepo, barabara ya Iringa iwepo. Zipo ‘open spaces’ nyingi zilizotengwa katika ‘Master Plan’ ya mwaka 1976”.
Aidha, ameiagiza halmashauri ya jiji hilo kuandaa na kuwasilisha ofisini kwake orodha na michoro yote ya maeneo ya wazi yaliyotengwa yaliyo wazi na ambayo yamevamiwa na watu.
Mkuu wa Mkoa alipiga marufuku wananchi kuvamia maeneo ya wazi na kujenga makazi na biashara za kudumu. “’Master plan’ ya mwaka 1976, kama ilionesha eneo ni ‘open space’ libaki kuwa ‘open space’. Zaidi ya hapo hatuwezi kuwa na Jiji la kisasa” alisema Dkt. Mahenge.
Wakati huohuo, aliwataka wakazi wa Dodoma kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi. “Napenda nitoe rai kwa wakazi wa Dodoma kujenga utamaduni wa kushiriki michezo na mazoezi. Michezo inasaidia kuimarisha afya na kujenga mwili” alisema Dkt. Mahenge.
Katika ziara yake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alitembelea na alikagua miradi ya kimkakati ya uboreshaji wa mandhari ya eneo la kupumzikia (Recreational park) katika eneo la Chinangali, ujenzi wa kituo kikuu cha mabasi na soko kuu katika eneo la Nzuguni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.