DENI la serikali ni himilivu, japokuwa hadi Novemba 30, 2019 limefikia Sh trilioni 54.84 sawa na ongezeko la asilimia 11.7 ikilinganishwa na Sh trilioni 49.08, Novemba 2018, imeelezwa.
Akizungumza jijini hapa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kati ya kiasi hicho, deni la nje ni Sh trilioni 40.39 na deni la ndani ni Sh trilioni 14.44.
Waziri Mpango alisema ongezeko la deni hilo, limetokana na riba ya mikopo, ambayo mikataba yake iliingiwa zamani na mikopo mipya yenye masharti nafuu na ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mpango alisema mikopo hiyo imetumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na viwanja vya ndege, ujenzi wa mitambo ya kufua umeme na utekelezaji wa miradi ya maji.
Alisema tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2018, inaonesha kuwa deni ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu, kwa kuzingatia vigezo muhimu vinavyotumika kimataifa.
Vigezo hivyo ni uwiano wa deni la serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 27.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 70.
“Uwiano wa deni la nje pekee kwa Pato la Taifa ni asilimia 22.2 wakati ukomo ni asilimia 55,” alisema.
Alisema uwiano wa deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 157.3 wakati ukomo ni asilimia 240. Dk Mpango alisema ulipaji wa deni la nje, kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 15.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 23.
Alisema hiyo ina maana kuwa Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli zake za maendeleo na kulipa mikopo, inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje kwa wakati.
Dkt. Mpango alisema Desemba 2019, serikali pia imefanya tathmini hiyo na matokeo ya awali hayatofautiani na tathmini ya Desemba 2018. Matokeo rasmi ya tathmini mpya, yatatolewa baada ya uchambuzi unaendelea kukamilika.
Chanzo: habarileo.co.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.