DIWANI wa Kata ya Majengo, Mhe. Msinta Mayaoyao amewataka wahitimu wa Chuo cha Uandishi wa Habari na Utangazaji Dodoma kuzingatia umakini na weledi katika kazi zao kutokana na umuhimu wa taaluma yao katika maendeleo ya nchi na ulimwengu kwa ujumla.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye Mahafali ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dodoma, katika hotuba yake aliwasisitiza wahitimu hao kuzingatia ukweli na usahihi wa maudhui wanayoyawasilisha kwenye mitandao ya kijamii na hata wawapo katika utekelezaji wao wa majukumu ya kazi. Alisema kuwa kufanya hivyo kutawajengea kuaminika na kuheshimika katika jamii.
Mhe. Mayaoyao alisema hayo kutokana na ongezeko kubwa la waandishi wanaosambaza taarifa ambazo hazijafanyiwa uchunguzi wa kitaaluma juu ya ukweli wa habari hizo. Kufanya hivyo kunapelekea jamii kutokuwa na imani na waandishi wa habari na taaluma ya habari kwa ujumla wake.
“Taaluma ya habari ni nyeti, na ni muhimu sana duniani. Tumieni elimu mliyoipata hapa ipasavyo, mkaoneshe utofauti kati ya ninyi wasomi na wale makanjanja wanaofanya kazi ili mkono uende kinywani. Endelezeni na mkawe mfano kama ilivyo kwa wakongwe wa tasnia hii”.
“Lakini kamwe hamuwezi kuwa waandishi wazuri kama mtakuwa hamjui kuutafuta ukweli wa jambo, kwani mnaweza kusababisha matatizo makubwa na hata kuwa chanzo cha migogoro miongoni mwa watu katika jamii,” alisema Mhe. Mayaoyao.
Mbali na hayo Diwani huyo alisisitiza juu ya kujenga uaminifu miongoni mwa jamii na ushirikiano, ili kurahisisha na kuwajenga wahitimu hao katika kuendea maisha ya mitaani hasa katika upande wa soko la ajira.
“Ushirikiano ni nguzo ya mafanikio, kokote muendako kumbukeni hili. Fanyeni kazi kwa kuzingatia miiko ya taaluma yenu, nidhamu pia itawabeba heshimianeni haijalishi ni mkubwa au mdogo. Simamieni misingi ya ukweli wa taarifa mkaonyeshe utofauti katika tasnia hii ya habari,” alisema Diwani huyo.
Chuo cha Uandishi wa Habari na Utangazaji Dodoma kilifanya mahafali yake ikiwa ni kwa mara ya pili, awamu ya kwanza kuyafanyia jijini hapa huku ya awamu iliyopita ikifanyika mkoani Morogoro.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.