Na. John Masanja, CHANG’OMBE
Diwani wa Kata ya Chang'ombe, Bakari Fundikira amefanya kikao na viongozi wa Soko la Mavunde chenye dhamira ya kuziangazia changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa soko hilo na kuzifanyia utatuzi.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Kata ya Chang'ombe iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya kikao hicho, Diwani Fundikira alisema moja ya changamoto walizozitambua ni pamoja na changamoto ya uwelewa wa mikataba pia kutozingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa shughuli za kibiashara ndani ya soko.
“Lengo letu sisi viongozi ni kuhakikisha kuna uelewa mzuri kwa wafanyabiashara hawa kuhusu jinsi ya kuendesha shughuli zao wakiwa kwenye mazingira rafiki kwa kuzingatia sheria na taratibu. Pia serikali yetu iweze kukusanya mapato pasipo mtu kushurutishwa wala kulazimishwa” alisema Diwani Fundikira.
Aidha, alitoa rai kwa wafanyabiashara kuendelea kutunza mazingira na miundombinu ya soko ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwataka wasisite kujitokeza pale inapoitishwa mikutano yenye kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo hususani utatuzi wa changamoto wanazokumbana nazo.
Kwa upande wake Afisa Biashara kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Erick Matiku alisema kuwa wafanyabiashara wengi wa Soko la Mavunde wamekuwa na changamoto ya utafsiri wa mikataba yao hali inayowapelekea kuingia kwenye migogoro isiyo ya lazima. Aliahidi kuendelea kutoa elimu zaidi kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Chang’ombe katika kuondokana na changamoto hizo.
Wakati huohuo, Mtunza Fedha wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Soko la Mavunde, Elizabeth Boniface alisema kuwa amekuwa akiwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi za Halmashauri kwa wakati.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.