SHILINGI bilioni 2.8 zinahitajika kwa ajili ya kufungua barabara kati ya Dodoma na Mbuga ya Wanyama ya Ruaha ili kuvutia watalii kutoka mkoani humo kwenda kuona vivutio katika hifadhi hiyo.
Meneja wa Tarura Wilaya ya Chamwino, Nelson Maganga alisema fedha hizo zikipatikana barabara hiyo itaboreshwa na kuwa katika kiwango bora cha kupitika wakati wote wa mwaka.
Maganga alisema, fedha hizo zikipatikana zitafungua barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 121 hadi Hifadhi ya Ruaha na hivyo kupunguza safari ya watalii kuzunguka Iringa kwenda umbali wa kilometa 368 kufika hifadhini.
Maganga alisema, barabara hiyo yenye kipande cha kilometa 30 za lami hadi Mpunguzi, itahitajika fedha za kurekebisha kipande cha kilometa 91 ili iwe katika kiwango bora cha kupitika msimu wote.
Tarura tayari wanaendelea na marekebisho kutokana na bajeti waliyopata mwaka jana 2018/19 ya Sh milioni 181 na ya mwaka huu 2019/20 ya sh milioni 171 katika kipande cha Manda hadi Mpunguzi.
Lakini kama fedha zingepatikana ingewezekana kuboresha kipande cha Manga hadi Ilangali kilometa 25 hadi kuwenda mpaka wa Dodoma na Iringa ili kuingia kwenye hifadhi hiyo.
Alisema juhudi za kufungua barabara hiyo zinafanyika kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge ambaye pamoja na wadau wengine amepita barabara hiyo na kushuhudia kwamba ni fupi sana kufika hifadhini.
Alisema Dkt. Mahenge anaendelea na mzungumzo na wizara ya maliasili na utalii ili kuona ni namna gani wanaweza kuunga mkono juhudi za mkoa kutaka kuifungua barabara hiyo ambayo ni muhimu katika kupeleka watalii kutoka Dodoma.
Alisema kabla ya kuingia kwenye hifadhi itatakiwa kujengwa karavati ambalo litarahisisha kuvuka na kuingia kuona wanyama katika hifadhi hiyo kupitia mkoani Dodoma.
Mkakati wa Mkuu wa Mkoa ni kualika wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii, taasisi ya TAWA, TANAPA, TAWIRI na taasisi nyingine kwa lengo kutembelea hifadhi kupitia njia hiyo ili kupiga picha na kutengeneza makala ambayo itauzwa kwa lengo la kupata fedha za kuboresha barabara na miundombinu mengine ili kufika hifadhini kwa njia hiyo fupi.
Barabara ya Dodoma - Mbuga ya Wanyama ya Ruaha ikiboreshwa itasaidia kuwapa fursa watalii wanaofika jijini Dodoma kupitia Uwanja wa Ndege wa Msalato, Reli ya Kisasa (SGR) na kupitia njia nyingine, hivyo watapata fursa ya kutembelea hifadhi hiyo yenye sifa ya kuwa na wanyama wengi kupitia Dodoma kuliko kuzunguka Iringa.
Chanzo: HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.