MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge ameridhishwa na utendaji kazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma hadi kupata hati safi katika ukaguzi wa hesabu za serikali za mwaka 2018/2019.
Kauli hiyo aliitoa katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa kupitia taarifa ya Mthibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa hesabu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2019 uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Mipango Dodoma.
Dkt. Mahenge alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepata hati safi kwa ukaguzi wa hesabu za mwaka 2018/2019. “Niwapongeze kwa dhati kwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kazi nzuri mliyoifanya kwa kipindi chenu cha miaka mitano mpaka Jiji la Dodoma linapendeza, hongereni sana. Hakuna kilichotekelezwa bila kupitia vikao vya Baraza la Madiwani, Baraza hili ni sehemu ya mafanikio yote yaliyofanyika hapa Dodoma. Hamuwezi kusahauliwa katika mafanikio ya hapa Dodoma” alisema Dkt. Mahenge.
Akiongelea hoja 46 za ukaguzi zilizopatikana, Mkuu wa Mkoa aliwataka kuzitatua hoja hizo. “Ukiziangalia hoja hizi za ‘CAG’, zaidi ya asilimia 80 ninyi wenyewe mnaweza kuzitatua. Ni asilimia ndogo tu ambayo ndiyo inahitaji ngazi ya juu kama upungufu wa watumishi kwenye sekta ya afya. Mnatakiwa kuweka mkakati na ratiba ya kuhakikisha hoja zote zinajibiwa. Hoja zilizo nje ya uwezo wa Jiji niwaahidi kama serikali ya Mkoa tutaendelea kushirikiana katika kuzitatua” aliongeza Dkt. Mahenge.
Akiwasilisha taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa hesabu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2019, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina jumla ya hoja 46 kwa mwaka 2018/2019. Katika hoja hizo, 12 ni za miaka ya nyuma na 34 ni hoja za mwaka 2018/2019. “Mheshimiwa mwenyekiti, tumeweza kupunguza hoja za ukaguzi kwa kiwango cha hoja 11 ukilinganisha na mwaka 2017/2018 ambapo tulikuwa na jumla ya hoja 57. Mheshimiwa mwenyekiti, hoja zote zimejibiwa na kuwasilishwa kwa Mkaguzi wa nje ndani ya siku 21 kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria” alisema Kunambi.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika ukaguzi wa hesabu za mwaka 2018/2019, Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za serikali ametoa hati safi. Hati hii inalifanya Jiji la Dodoma kuendelea kupata hati safi toka mwaka 2016/2017 hadi 2018/2019.
Aidha, mwaka 2018/2019 aliutaja kuwa ni mwaka wa pekee wa kujivunia. “Nichukue nafasi hii kuipongeza kwa dhati kabisa timu yangu mahili ya wakuu wa Idara na Vitengo wa Jiji la Dodoma. Kweli wamefanya kazi nzuri. Maana msingi wa hoja unatoka kwenye idara na mimi kama afisa masuuli ninafanya matumizi ya idara zote, kama mkuu wa Idara asipokuwa makini kunishauri kwenye eneo lake tunatengeneza hoja nyingi sana. Haya ni matokeo ya kazi bora iliyotukuka” alisisitiza Kunambi.
Akiongelea siri ya Jiji kupata hati safi, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa hati safi ni ishara ya utekelezaji shughuli za maendeleo usio na shaka. “Maendeleo yanakuja mahali palipo na amani, sisi tumetulia na maendeleo yapo. Hizi hoja tunaamini zitakuwa zinabadilika kadri tunavyoendelea na zitakuwa labda zinabaki zile za kisera pakee. Nidhamu ya kutii sheria, kanuni na taratibu ndiyo msingi wa mafanikio” alisema Prof. Mwamfupe.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Patrobas Katambi alisema kuwa mipango ya maendeleo inatolewa na serikali kupitia Ilani ya CCM na kwenye utekelezaji inaingia kwenye mfumo wa serikali wa ufuatiliaji, usimamizi na utendaji. “Ufuatiliaji na usimamizi unafanywa na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya. Kwenye utendaji, unakuja kwenye ngazi ya Halmashauri pamoja na Baraza la Madiwani ambalo hilohilo pia linasimamia utekelezaji wake. Hivyo, hati safi maana yake ni ufuatiliaji, usimamizi na utekelezaji vinafanyika kwa usahihi” alimalizia Katambi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.