WAZIRI wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Phillip Mpango ametokea hadharani na kuwapongeza Wataalam wa Afya katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa huduma bora wanazotoa hasa katika kipindi alichokuwa hospitalini hapo akipata huduma ya matibabu.
Waziri Mpango amesema “…Madaktari, manesi, wataalam wa viungo, mpaka wahudumu, yaani kila mtu wanafanya kazi usiku na mchana kwa tabasamu, kwa upendo wa ajabu, yaani huduma mimi niliyopata hapa, menejimenti ya hospitali yetu huduma hizi ndugu zangu watanzania ni huduma bora sana, sana madaktari hawa, unawaona ni vijana, sijui nitumie neno gani ‘excellent professional service’”. Alisema Dkt. Mpango kwa msisitizo.
Aidha, aliweka wazi kuwa kulikuwa na vishawishi, vya kumtaka kuhamia Dar es Salaam au mahali pengine ili akapate matibabu lakini alisema hapana. “…hakuna nilichokosa hapa kabisa kabisa, hospitali hii ni nzuri sana, vifaa ni vya kisasa kabisa, kama nilivyosema hawa ni madaktari kweli kweli, wameiva and I am proud kutibiwa na madaktari vijana wa kitanzania”.
Akifafanua Zaidi alisema kuwa sababu ya kumbilia Ulaya hata pamoja na hali ya sasa, haipo. Sisi tuelekeze nguvu kuboresha hospitali zetu hapa nchini, na amesisitiza kuwa katika nafasi ambayo Mwenyezi Mungu amemjalia kupitia uteuzi wa Rais anajisikia vizuri kwamba wakati wake kama waziri wa fedha wameweza kuelekeza fedha nyingi zaidi kuboresha huduma za afya kuanzia ujenzi wa hosptali, vituo vya afya, zahanati, dawa, kusomesha madaktari na kadharika. Dkt Mpango akasema kuwa anasikia furaha sana kwa utekelezaji huo wa Serikali.
Vile vile ameahidi kuwa kwa nafasi aliyonayo ataendelea kwa nguvu zaidi, kumshauri Mheshimiwa Rais kuelekeza nguvu zaidi na zaidi kwenye sekta ya afya ambayo inagusa sana wanyonge watanzania.
“Lazima tuboreshe zaidi bajeti ya wizara (Afya), lazima tuangalie mahitaji muhimu ya hospitali kama hii (Hospitali ya Benjamin Mkapa) iliyopo makao makuu ya nchi yetu na hospitali nyingine za hapa Dodoma, lazima tuangalie maslahi na mahitaji ya msingi ya wataalam wetu hawa wazalendo muhimu sana, manesi madaktari wote, lazima tuyaangalie upya” alisema Waziri huyo kwa kujiamini.
Akielezea Zaidi alisema kuwa kuugua kwake na kuugulia Hospitali ya Benjamin Mkaa imempa fursa na upeo katika nafasi yake ya ushauri, ya kushauri namna ambavyo kama nchi tunaweza tukafanya vizuri zaidi katika eneo la utoaji wa huduma za afya nchini.
“Nataka niwaambie watanzania afya yangu imeimarika vizuri kabisa na hatimaye jopo la madaktari wameona nina afya njema, na nina uwezo wa kurudi kuendelea na shughuli za kulitumikia taifa letu”. Alisema Dkt. Mpango kwa kujiamini.
Mwisho alitoa shukrani, kwanza ni kwa Mwenyezi Mungu aliyetuumba watu wote, kwa amemtendea makubwa, (kutoka siku 14 ambazo madaktari walikuwa wakimhudumia nyumbani na baadae wakaona wamhamishie Hospitalini Benjamin Mkapa, “acheni Mungu aitwe Mungu, tuendelee kumtukuza na kumuomba yeye aliye muweza wa yote”.
Pili kwa nafasi ya pekee sana amemshukuru sana Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na familia yake, kwa kumpigia simu kila siku akimjulia hali na alikuwa akituma wasaidizi wake kufuatilia maendeleo yake siku kwa siku. Nawashukuru pia Watanzania wote na viongozi wa dini na wote.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.