MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ili kupata manufaa ya maadhimisho ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, ni lazima kuacha kufanya maadhimisho hayo kimazoea bali yalenge kubadili fikra na mwenendo wa wananchi wanapotumia barabara.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani na Maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma. Amesema ukaguzi wa magari unapaswa kuwa endelevu na kufanyika kwa mwaka mzima badala ya kusubiri hadi kwenye Wiki ya Usalama barabarani Kitaifa.
Makamu wa Rais amesema kwa kuwa makosa ya kibinadamu ndiyo chanzo kikubwa cha ajali nchini, hakuna budi kuelekeza nguvu katika kudhibiti vihatarishi mahsusi vitano ambayo ni mwendo kasi, kuendesha chombo cha moto katika hali ya ulevi, kutovaa kofia ngumu, kutofunga mikanda ya usalama katika gari pamoja na ukosefu wa vifaa vya usalama kuwalinda watoto wadogo wawapo ndani ya magari.
Aidha ametoa rai kwa wananchi na hasa abiria katika vyombo vya usafiri kukemea au kutoa taarifa za uvunjifu wowote wa Sheria za Usalama Barabarani, hususan kuhusu uendeshaji wa mwendokasi na usio salama au uharibifu wa barabara na miundombinu yake.
Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa udhibiti wa magari yanayobeba wanafunzi kwa kuwa magari mengi yana hali mbaya inayotishia usalama wa wanafunzi na madereva wenyewe. Amesema baadhi ya madereva wa magari hayo wameonekana kukosa weledi na uadilifu hali inayosababisha madhara mbalimbali zikiwemo ajali mbaya.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuwekeza katika TEHAMA ili kudhibiti kirahisi ajali na makosa mengine ya usalama barabarani. Pia amesisitiza kuongeza jitihada katika kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia njia mbalimbali hususan vyombo vya habari, machapisho mbalimbali, maonesho, sanaa na muziki, mikutano ya hadhara pamoja na njia ya mitandao ya kijamii ili kuyafikia makundi yote ya watumiaji wa barabara.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.