MAKATIBU Tawala wa Mikoa nchini wametakiwa kuhakikisha wakuu wa shule za msingi na sekondari na waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya wanapewa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa manunuzi (NeST) kabla ya kuanza kutumika.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa itaongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi hasa ikizingatia kuwa Serikali inakusudia kupeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika maeneo hayo.
Maagizo hayo yametolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Charles Msonde wakati wa kufungua mafunzo ya mfumo wa ununuzi wa umma (NeST) yanayofanyika katika Ukumbi wa shule ya msingi Mtemi Mazengo Jijini Dodoma.
Alisema Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi za kutekeleza miradi katika ngazi ya mzingi hivyo Ma-RAS, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa idara ya halmashauri kuhakikisha wanafundisha kwa ukamilifu wale wote wanaotekeleza shughuli za manunuzi katika ngazi ya msingi wakiwemo wakuu wa shule na waganga wafawidhi.
“Mkifanya hivyo shughuli za manunuzi zitakwenda vizuri, thamani ya fedha itaonekana kwenye miradi na itakamilika kama vile ambavyo serikali inataka.”
Pia amewataka wataalamu wote watakaohusika katika mchakato wa manunuzi kuhakikisha wanazingatia matumizi ya mfumo huo ili kujiepusha na makosa ambayo yanaweza kuwatia matatani.
Mafunzo hayo yamefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa ya kuhakikisha wataalamu katika serikali za mitaa wanatumia mfumo wa manunuzi wakati wa kutekeleza miradi ya ujenzi katika maeneo yao.
“Ukiwa hapa usijadili kama mtu wa Dodoma bali mwakilishe wengine ambao hawako hapa kutoka mikoa yote ya Tanzania, hivyo mnapopewa mafunzo haya myasikilize vizuri na myaelewe, palipo na utata mseme ili msije kupitisha vitu ambavyo kiuhalisia havitekelezeki,” amesema Dkt. Msonde wakati wa kusisitiza umakini wa washiriki wa mafunzo hayo.
Awali, Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Erick Kitali amesema idara yake itaendelea kuwekeza katika kuboresha na kubuni mifumo ambayo ni rafiki kwa matumizi kwa manufaa ya serikali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.