Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison George Mwakyembe amezitaka Halmashauri za Wilaya nchini kupeleka walimu wa michezo kwenye chuo cha michezo cha Malya kilichopo Mwanza ili kuboresha weledi wa walimu hao katika michezo nchini.
Mhe. Dkt Mwakyembe ameyasema hayo wakati akifungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) mwaka 2019 yanayofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara.
Amesema kila akitembelea chuo cha Malya, hukuta walimu wengi wanaosoma pale hujilipia wenyewe badala ya kulipiwa na serikali jambo alilosema kuwa siyo sawa kwani walimu wanaosoma Malya siyo kwa faida yao pekee bali ni kwa ajili ya maendeleo ya michezo ya halmashauri wanakotoka.
Hivyo, Dkt. Mwakyembe amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa wanatenga fedha kwa ajili ya kusomesha walimu wake wanaotaka kujiendeleza katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kwa ajili ya kuboresha weledi wao katika fani ya michezo.
“Nitakapotembelea tena chuo cha Malya nikikuta wapo walimu ambao wanajilipia wenyewe kwa fedha zao nitahakikisha kuwa Halmashauri wanakotoka walimu hao tunazitangaza ili nao wapate aibu,” amesema.
Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Halmashauri zinatenga fedha kwa ajili ya shughuli nyinginezo mfano fedha za chai lakini zinaona ugumu kutenga fedha kwa ajili ya kupeleka walimu Malya kusomea fani ya michezo.
Akizungumzia kuhusu ufunguzi wa mashindano ya UMITASHUMTA Dkt. Mwakyembe ameelezea furaha yake kuona kuwa katika mashindano ya mwaka huu vipengele vya burudani ya ngoma vitashindanishwa na kuongeza kuwa fani hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa kwani katika bajeti ya mwaka huu sanaa na burudani vimechangia kwa asilimia kubwa pato la taifa.
Aidha Mhe. Mwakyembe ameagiza kuwa kila shule iliyosajiliwa nchini kuanzia ile ya chekechea ihakikishe kuwa inazingatia kuimbwa kwa wimbo wa taifa kila siku asubuhi.
Kuhusu mashindano ya UMITASHUMTA, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa mashindano hayo ni muhimu sana katika kuibua vipaji vya wanafunzi ambao siku za usoni watakuja kuliletea heshima taifa letu.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa vipaji hivyo kuviibua, na kuvilea ili vije kuleta matunda yanayokusudiwa kwa taifa letu.
Amesema kuwa michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA ni muhimu sana kwa ukuaji wa sekta ya michezo katika taifa huku akitolea mfano jinsi vijana walioibuliwa na kuandaliwa vyema baada ya michezo ya UMISSETA iliyofanyika Mwanza walivyoweza kuliletea heshima kubwa taifa letu katika mchezo wa riadha baada ya kuibuka na medali 13 na hivyo kushika nafasi ya kwanza miongoni mwa nchi 11 zilizoshiriki mashindano ya ukanda wa tano wa mchezo wa riadha duniani.
Aidha, Dkt. Mwakyembe ameupongeza Mkoa wa Simiyu kwa kuanzisha shule maalum ya michezo ambayo itakuwa shule ya kwanza ya umma itakayokuwa na jukumu la kuendeleza michezo na elimu nchini.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amesema kuwa mkoa wa Simiyu uliamua kuja na wazo la kuanzisha shule ya michezo kwa lengo la kulea vipaji vya michezo shuleni.
Amesema kuwa shule hiyo inatarajiwa kuanza mwaka ujao wa masomo ambapo wataanza kwa kuchukua watoto 120 katika mwaka wa kwanza na baada ya hapo watakuwa wakichukua wanafunzi 80 kila mwaka.
“Shule hii zamani ilikuwa ni ya kutwa, tumeigeuza kuwa ya bweni na inaitwa Shule ya Sekondari Simiyu. Tunatarajia kuwa na jumla ya wanafunzi 320 ambapo vijana watakaokuwa wakifaulu mitihani yao ya darasa la saba na wenye vipaji vya michezo wataletwa moja kwa moja katika shule hii,” amesema.
Naye Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Benjamin Oganga amesema kuwa Mashindano ya Michezo ya UMITASHUMTA Taifa kwa mwaka 2019 yameshirikisha Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ambapo jumla ya wanafunzi 2,600, walimu na viongozi 675 wanashiriki michezo hii.
“Michezo wanayoshiriki wanafunzi hawa ni mpira wa miguu, netiboli, mpira wa mikono, mpira wa wavu, riadha jumuishi na mpira wa goli (kwa wasioona na wenye uoni hafifu) na fani za ndani zitakazohusisha Kwaya na Ngoma,” amesema.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mashindano hayo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema kuwa mkoa wake umejiandaa kuwapokea na kuwakarimu watoto na wageni wote waliofika Mtwara huku akiamini kuwa watoto wanahitaji upendo, ukarimu na kuelekezwa.
Mara baada ya ufunguzi wa mashindano hayo kulichezwa mchezo wa mpira wa miguu baina ya timu ya soka wavulana kutoka mkoa wa Lindi dhidi ya majirani zao timu ya mkoa wa Mtwara ambapo mechi hiyo baada ya dakika 60 kuchezwa timu ya soka kutoka mkoa wa Lindi ilifanikiwa kuinyuka timu ya soka ya mkoa wa Mtwara kwa magoli 2-0. Magoli ya washindi yalifungwa na Arid Ramadhani na Omary Mohamed ambaye alifunga goli la pili kwa njia ya penati.
Mashindano ya UMITASHUMTA yatafanyika kwa muda wa wiki mbili na yameshirikisha mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na yanatarajiwa kufungwa tarehe 3 Julai, 2019 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo katika uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara. Halmashauri ya Jiji la Dodoma inawakilishwa na timu za mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha na ngoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.