RAIS mteule wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ally Hassan Mwinyi ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa awamu ya nane.
Mwinyi amekula kiapo leo Jumatatu Novemba 2, 2020 katika uwanja wa Amani mjini Unguja, zilipofanyika sherehe za kuapishwa kwake.
“Mimi Hussein Ali Mwinyi, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Zanzibar na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba, nitaihifadhi, nitailinda, nitaitii na kuitetea Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake kwa mujibu wa sheria iliyowekwa,” ndivyo alivyoapa kiongozi huyo.
Baada ya kuapa Rais Mwinyi aliahidi kuwa na utendaji kazi wenye viwango bora na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha huduma za kijamii kwa kuzitumia vyema rasilimali za Zanzibar kwa manufaa ya wananchi.
Akitoa ahadi ya kushirikiana na vyama vya upinzani Dkt. Mwinyi alisema "Ndugu zangu ninawapongeza wagombea wenzangu kwa nafasi ya urais ambao wameyakubali matokeo ya uchaguzi na kuheshimu maamuzi ya wananchi na ninatoa ahadi ya kuwa nitashirikiana nao katika Serikali nitakayoiunda katika kuwatumikia wananchi na kuijenga Zanzibar".
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alipata wasaa wa kusalimianana na viongozi mbalimbali waliokaa kwenye jukwaa kuu wakiwamo marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dkt. Ali Mohamed Shein pamoja na marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi (ambaye ni baba yake mzazi) na Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Awamu ya nne wa Muungano.
Dkt. Mwinyi anaanza uongozi wake wa miaka mitano baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba 27 na 28, 2020 akimrithi mtangulizi wake Mhe. Ali Mohamed Shein aliyemaliza muda wake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Hassan Mwinyi (wa pili kulia) akisalimiana na Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ally Hassan Mwinyi (ambaye pia ni baba yake mzazi) mara baada ya kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Zanzibar.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.