Na. Dennis Gondwe, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi 14,482,250,000 kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kuanzia sekta za afya, elimu, ardhi, viwanda hadi uwekezaji miradi iliyosaidia kuboresha huduma zakijamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akiongelea mafanikio ya miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ofisini kwake.
Mafuru alisema katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa jumla ya shilingi 14,482,250,000 kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za Afya, Elimu, Ardhi na Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Aidha, Mheshimiwa Rais anaendelea kutekeleza miradi mingine mikubwa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambayo ni ujenzi wa Barabara ya mzunguko, ujenzi wa reli ya kisasa ya mwendokasi na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.Miradi yote hii imelenga kuboresha maisha ya wananchi.
Akiongelea sekta ya elimu, Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa halmashauri yake ilipokea shilingi 3,520,000,000 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 172 na samani zake.Shilingi 954,000,000 zimepokelewa kutoka kwa wahisani wa SEQUIP kwaajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Mtemi Chiloloma, mabweni mawili na madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Bihawana. Mabweni mawili, madarasa mawili na madawati 60 katika shule ya sekondari ya wasichana ya Bunge alisema Mafuru.
Alisema kuwa shilingi 750,000,000 zimepokelewa kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwaajili ya ujenzi wa shule mpya ya mchepuo wa kingereza (Msangalale English Medium). Eneo lingine lililopokea fedha shilingi 858,250,000 ni kwaajili ya uboreshaji miundo mbinu ya elimu ya msingi, aliongeza.
Mafuru alisema kuwa fedha zilizotolewa na serikali ya awamu ya sita kwa halmashauri yake ni nyingi kwaajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Alisema kuwa fedha hizo zitaleta mapinduzi makubwa katika huduma za jamii na maendeleo ya watu na halmashauri yake. Aliahidi kuendelea kusimamia fedha hizo ili zilete matokeo makubwa na kuonesha thamani ya fedha kwenye miradi hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.