MKOA wa Dodoma umeandaa kongamano la uwekezaji kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwa lengo la kuvutia wawekezaji katika maeneo mbalimbali na kukuza uchumi wa mkoa huo.
Kauli hiyo ilimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa akitoa maelezo muhimu kuhusu Kongamano la Uwekezaji la Mkoa wa Dodoma kwa mgeni rasmi Waziri Mkuu wa Tanzania katika ukumbi wa Dodoma Convention Centre.
Dkt. Mahenge alisema “katika kufikia azma ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda, Mkoa wa Dodoma umeandaa kongamano hili la uwekezaji kwa lengo la kutangaza fursa na vivutio vya uwekezaji vilivyopo katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi”.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Mkoa wa Dodoma unazo sifa zinazoufanya uvutie kwa uwekezaji. Sifa hizo alizitaja ni kuwa makao makuu ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Fursa kubwa ya uwepo wa soko la bidhaa mbalimbali zitakazozalishwa hapa na soko kubwa la mahitaji ya huduma za jamii kutokana na idadi kubwa ya watu wanaohamia Dodoma wenye kipato cha kati na kikubwa. Wageni kutoka mataifa mbalimbali, mabalozi na taasisi za kimataifa. Fursa nyingi za uwekezaji na biashara kwenye ujenzi wa makao makuu mapya ya nchi katika karne ya 21 ya sayansi na teknolojia za kisasa” alisema Dkt. Mahenge. Wawekezaji na wafanyabiashara hawahitaji kufanya utafiti wowote ili kufanya biashara kutokana na ukweli kwamba makao makuu ya nchi mahitaji ya hoteli za kisasa, nyumba za wageni, huduma za afya za kisasa na shule za kimataifa hayakwepeki, aliongeza.
“Napenda kwa niaba ya serikali, Mkoa na wananchi kutoa pongezi na shukurani kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake thabiti wa kuhamishia makao makuu ya serikali mkoani Dodoma, jambo ambalo ni kichocheo na chanzo kikuu cha fursa nyingi za uwekezaji” alisema Dkt. Mahenge.
Akiongelea uboreshaji mazingira ya uwekezaji mkoani Dodoma, Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimefungua ofisi ya kanda ya kati jijini Dodoma.
“Huduma mbalimbali zikiwepo kupata taarifa na taratibu za uwekezaji, maombi ya vibali na leseni mbalimbali za uwekezaji kwa wawekezaji wanaowekeza Dodoma zinaratibiwa na ofisi hii. Wawekezaji wa ndani na nje wamechangamkia fursa hii ambapo kwa kipindi cha mwezi Julai 2016 hadi Juni 2019, jumla ya miradi mipya 22 imesajiliwa katika Mkoa wa Dodoma ambayo inatarajia kuwekeza mtaji wa Dola za Marekani 232.51 Milioni na kuzalisha ajira mpya 2,867” alisema Dkt Mahenge.
Suala la usafiri si kikwazo kwa Mkoa wa Dodoma. Alisema kuwa mkoa huo umeunganishwa na miundombinu ya usafiri na usafirishaji mizuri kwa barabara za lami zinazounganisha na mikoa mingine, na kiwanja cha Ndege. “Ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji unaendelea sasa: SGR, barabara za pete ya ndani na nje, uwanja wa kimataifa wa ndege Msalato, stendi ya kisasa na soko” alisisitiza Dkt. Mahenge.
Kongamano la Uwekezaji Mkoa wa Dodoma litafanyika kwa siku mbili likiongozwa na Kaulimbiu isemayo “Dodoma fursa mpya ya kiuchumi Tanzania, wekeza Dodoma, tukufanikishe”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.