WAZIRI mkuu mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda amepongeza kazi nzuri ya maendeleo iliyofanywa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli katika Jiji la Dodoma.
Pongezi hizo alizitoa alipokuwa akisalimia mamia ya wananchi wa Dodoma katika uwanja inapojengwa stendi kuu ya mabasi eneo la Nzuguni jijini Dodoma jana.
Pinda alisema “napenda kutoa pongezi kwako Mhe Rais na Serikali yako kwa kazi nzuri na kubwa inayofanyika nchini kwetu, tunakupongeza sana. Mimi nimeanza kuja Dodoma mwaka 1978, Dodoma imebadilika sana! Kazi iliyofanywa ndani ya miaka minne inatisha zaidi. Tunakuombea kwa Mungu aendelee kukuongoza, akupe hekima na busara katika kuwatumikia watanzania”.
Jiji la Dodoma linaenda kwa kasi kubwa sana, aliongeza. Kufuatia kasi ya ukuaji wa Jiji la Dodoma, Waziri mkuu huyo mstaafu aliongelea changamoto ya upatikanaji wa Maji ya uhakika. “Hofu yangu ipo eneo la upatikanaji wa Maji. Changamoto bado ni kubwa. Tegemeo kubwa ni chanzo cha Maji kimoja tu eneo la Makutopola. Kwa ukuaji wa Jiji, chanzo hicho kinaweza kisimudu” alisema Pinda. Aidha, alishauri kuwa mradi mkubwa wa Maji kutoka ziwa Victoria kwenda mikoa ya Shinyanga na Tabora utengenezewe mfumo ili uweze kufika mikoa ya Singida na Dodoma.
Waziri mkuu mstaafu alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa katika halfa ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa soko kuu la Dodoma na stendi kuu ya mabasi eneo la Nzuguni jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.