Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selamani Jafo amesema mazingira ndiyo ajenda inayosababisha uchumi kuwa imara.
Amesema hayo wakati akizungumza na wanafunzi kutoka shule mbalimbali, viongozi na wananchi walioshiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la Medeli jijini Dodoma leo Februari 7, 2022.
Dkt. Jafo alisema kuwa uchumi imara ni matokeo ya utunzaji mazingira kwa kuwa ni chanzo cha mvua ambazo zinasaidia kujaa kwa maji katika mabwawa ya kufua umeme ambao hutumika katika viwanda.
“Ndugu zangu tukikosa mvua tutakosa umeme na tukikosa umeme viwanda vitashindwa kufanya kazi na vikishindwa kufanya kazi watu watakosa ajira na watu wakikosa ajira uchumi utaporomoka kwa hiyo agenda ya mazingira inasababisha hata uchumi kuweza kuwa imara,” alisema.
Zoezi hilo ambalo ni miongoni mwa shughuli zinazofanyika kuelekea uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 unaotarajiwa kufanywa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango Februari 12, 2022.
Pia, Waziri Dkt. Jafo alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kutumia mvua zinazonyesha katika maeneo mbalimbali nchini kupanda miti ili ikue na ambayo itasaidia katika kurejesha mazingira katika hali nzuri.
Aliwashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza na kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais wakiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wanafunzi na wananchi kwa ujumla kushiriki katika zoezi hilo.
Aidha, waziri huyo alihamasisha wanafunzi hao kupeleka ujumbe kwa wazazi wao kushiriki katika zoezi la kupanda miti katika maeneo yao ili kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga alisema katika zoezi hilo wameweza kupanda aina mbalimbali za miti ikiwemo ya matunda na kivuli.
Bi. Maganga alisema kuwa zoezi hilo limekwenda vizuri na watu wamejitokeza kwa wingi kushiriki kupanda miti pamoja na kuwepo kwa changamoto ya kuwepo kwa mvua.
Serikali imeamua kuwa na Wiki ya Uzinduzi wa Sera iliyoanza leo Februari 7, 2022 ambayo inaambatana na shughuli mbalimbali za hifadhi ya mazingira ikiwa ni sehemu ya masuala ya msingi yanayoelekezwa katika Sera mpya.
Ikumbukwe kwamba Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 imeongeza wigo wa masuala na changamoto za mazingira zinazopaswa kufanyiwa kazi katika kipindi husika ili kuleta maendeleo endelevu na imezingatia changamoto mpya za kimazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira yanayoendelea duniani.
Dhumuni la kuwepo kwa shughuli hizo ni kurejesha hali ya asili ya mazingira iliyoharibika kutokana na shughuli za kibinadamu kwa kuwa na zoezi la upandaji miti, kuboresha afya ya jamii na elimu ya utenganishaji taka kwa ajili ya udhibiti wa taka ngumu na kuwezesha urejelezaji wa taka kwenye bidhaa na huduma mbalimbali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.