HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imesajili wanachama 330 katika siku yake ya kwanza ya utekelezaji wa zoezi maalum ya uhamasishaji wananchi kujiunga na Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (CHF) katika Kata ya Chang’ombe mwishoni mwa wiki hii.
Akizungunza na wanahabari baada ya zoezi hilo mratibu wa CHF iliyoboreshwa Patrick Sebyiga alisema kuwa zoezi hilo limeanza kwa mafanikio makubwa katika Kata ya Chang’ombe kutokana na mwitikio wa wananchi kuwa mzuri.
Sebyiga alisema kuwa idadi ya kaya zilizosajiliwa ni 55, zenye jumla ya watu 330. “Katika Kata ya Chang’ombe muitikio wa watu ni mkubwa na hii imetupa picha kuwa zoezi la usajili linatakiwa kuendelea katika Kata hiyo” alisema Sebyiga.
Mratibu huyo alisema kuwa hoja nyingi za wananchi zilikuwa zinajikita katika iliyokuwa CHF ya awali. “Timu yangu ya wataalam na wahamasishaji imeendelea kuwaelimisha wananchi tofauti ya CHF ya awali na CHF hii iliyoboreshwa na baada ya kuelewa wananchi wamekuwa wakijiunga” alisema mratibu huyo.
Akiongelea tofauti baina ya CHF ya awali na iliyoboreshwa, alisema CHF iliyoboreshwa huduma zake zimeboreshwa. “CHF ya awali ilikuwa usajili unafanyika kwa kujaza fomu na baada ya hapo unasubiri mwezi mmoja ndipo uanze kupata huduma ya matibabu. Kwa CHF iliyoboreshwa ni ya kidigitali ambayo usajili na kadi yako unapewa papohapo na huduma ya matibabu kuanza mara moja” alisema Sebyiga.
Tofauti nyingine aliitaja kuwa CHF iliyopita walengwa wengi walikuwa hawapati huduma ya tiba na dawa katika vituo vya afya. “Sasa huduma zimeboreshwa zaidi. Matibabu hutolewa kuanzia ngazi ya Zahanati. Pale ambapo mgonjwa anahitaji rufaa basi utaratibu wa rufaa hufanyika kwenda kituo cha Afya, Hospitali ya Wilaya hadi hospitali ya rufaa ya Mkoa. Hii yote ni kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Magufuli za kumhakikishia mwananchi huduma bora za matibabu. Matibabu sasa ni nchi nzima katika vituo vya afya na hospitali za serikali” alisema Sebyiga.
Mratibu huyo alisema kuwa zoezi la uhamasishaji ni endelevu litakalofanyika katika Kata zote 41 za Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.