Na. Mussa Richard, DODOMA
Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, imejiandaa kuwakabili Klabu ya soka ya Tanzania Prisons katika muendelezo wa mbilinge mbilinge za duru ya pili ya Ligi kuu ya NBC Tanzania bara hapo kesho katika dimba la Jamhuri Dodoma.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Tanzania Prisons, Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Meck Mekisime alisema “Timu ipo tayari na tumejiandaa vizuri tukijua kuwa mchezo utakua mgumu kwasababu wapinzani wetu wametoka kupoteza michezo miwili mfululizo. Kwahiyo, sisi kama klabu tupo tayari kupambana na kuhakikisha alama tatu zinabaki Dodoma na niwaombe mashabiki na wanadodoma kwa ujumla kesho waje kwa wingi uwanjani kuja kuwaunga mkono wachezaji na kuwafariji kutokana na kile kilichotokea siku kadhaa zilizopita, jambo ambalo litawaongezea nguvu wachezaji kuipambania timu huku wakijua kuna namba kubwa ya watu jukwaani inawaunga mkono”.
Nae, Augustin Nsata, Nahodha wa klabu ya Dodoma Jiji FC, akaelezea hali ya utimamu wa wachezaji kuelekea katika mchezo huo. “Kama wachezaji morali ni kubwa na tupo salama kiakili na kimwili kuelekea katika mchezo huo, na kila mchezaji anautaka mchezo na yupo tayari kuipambania nembo ya klabu, kikubwa tuwaombe mashabiki waje kwa wingi uwanjani kutuunga mkono vijana wao ili kwa pamoja tuhakikishe tunashinda mchezo huu na kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa ligi na kila mchezo kwasasa kwetu ni fainali” alisema Nsata.
Kuelekea mchezo huo Dodoma Jiji FC, imeanzisha kaulimbiu inayoitwa Mchezo wa Shukrani ambapo Dodoma Jiji FC, itatumia mchezo huo kumshukuru Mungu kutokana wachezaji wake, maafisa na benchi lake la ufundi kunusurika katika ajali waliyoipata wiki iliyopita wakati timu ikitokea mkoani Lindi ambapo ilitoka kulazimishwa sare na Namungo FC.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.