TIMU ya soka ya Dodoma Jiji FC iliyo chini ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kesho Jumamosi Julai 11, 2020 itatupa karata ya kihistoria katika uwanja wa Jamhuri Jijini humo ambayo itaamua endapo timu hiyo itafuzu moja kwa moja kupanda Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara inayodhaminiwa na kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom kwa msimu ujao au vinginevyo kwa kukabiliana na Iringa United ya mkoani Iringa.
Mchezo huo wa mwisho wa ligi daraja la kwanza kwa msimu huu unatarajiwa kupigwa saa 10:00 jioni, na unatarajiwa kutoa hatma ya Dodoma Jiji FC kwani ili ifuzu italazimika kushinda ili kujihakikishia kupanda Ligi Kuu msimu ujao na endapo itapoteza itasubiri kupata matokeo ya mchezo mwingine wa kundi A kati ya Ihefu FC ya Mbarali Mbeya itakayokuwa kibaruani dhidi ya Cosmopolitan ya Dar es Salaam kwenye dimba la Highland Estates lililopo katikati ya mashamba ya mpunga huko Ubaruku Wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya.
Mpaka sasa Dodoma Jiji inaongoza kundi mbele ya Ihefu kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa huku timu zote zikiwa na pointi 48, hali iliyopelekea ushindi wa aina yake katika kundi hilo mpaka hapo michezo ya mwisho inayopigwa mwishoni mwa wiki hii itakapoamua mbivu na mbichi tofauti na kundi B ambapo timu ya Gwambina FC ya Misungwi mkoani Mwanza ilishafuzu kucheza Ligi Kuu msimu ujao ikiwa na michezo kadhaa ‘mkononi’.
Akizungumzia mchezo wa kesho, Afisa Habari Dodoma Jiji FC Ramadhani Juma amesema kikosi chao kimeandaliwa vizuri kimwili na kiakili kuhakikisha kinawapa raha wana Dodoma baada ya kukosa uhondo wa Ligi Kuu kwa takrabani misimu nane katika Jiji hilo.
“Kocha Mkuu Mbwana Makata akishirikiana na wasaidizi wake Renatus Shija na Mfaume Athumani wamekiandaa kikosi tayari kwa ‘vita ya kesho, ni mchezo wa kihistoria ambao utairudisha Dodoma kwenye ligi kuu ya Tanzania” alisema Juma.
Alisema maandalizi yote ya mchezo huo yamekamilika na kinachosubiriwa ni muda tu, na kwamba ushirikiano wa wadau wote ni muhimu katika kipindi hiki ili kufikia lengo la kupanda daraja kwa timu hiyo.
“Kwanza kwa niaba ya uongozi na Halmashauri ya Jiji kwa ujumla nitoe shukran nyingi sana kwa wapenzi na wadau wa timu na wakazi wote wa Dodoma kwa ushirikiano na mapenzi makubwa waliyoyaonesha kwa timu yao tangu mwanzo wa ligi, tumefika hapa leo kwa juhudi na ushauri wao katika kuiunga timu mkono” alisema.
Juma alitoa wito kwa wakazi wa Dodoma na Wilaya zake kufurika kwa wingi kesho kwenye uwanja wa Jamhuri ili kukamilisha kazi waliyoianza Septemba mwaka jana.
“Ni mchezo wa kihistoria hivyo nadhani kila mwana Dodoma ahakikishe anakuwa sehemu ya historia hiyo kwa kuja uwanjani ili kuwapa nguvu ya kupambana wachezaji wetu ambao wamekuwa wakipigana katika mchezo kwa nguvu zao, mchezo utaanza saa kumi kamili jioni na kiingilio itakuwa shilingi elfu (2,000) tu” alisistiza.
Timu hiyo ilichukuliwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoka wadau ambao walipambana kuipandisha daraja kwa misimu miwili iliyopita lakini hawakufanikiwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.