Timu ya Dodoma Jiji FC inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza nchini msimu wa 2019/20 baada ya kuifunga timu ya Gwambina FC kutoka Jijini Mwanza katika mchezo wa fainali uliofanyika katika uwanja wa Azam Complex Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Dodoma Jiji walijihakikishia ushindi huo kwa bao la pekee la ushindi lililofungwa na mshambuliaji wake hatari Anuary Jabir katika dakika ya 52 ya mchezo baada ya kuwahadaa walinzi wa Gwambina.
Gwambina ilifanikiwa kutinga fainali hiyo baada ya kukata tiketi ya kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21 baada ya kuongoza kutoka kundi B la Ligi Daraja la Kwanza.
Nayo Dodoma Jiji FC iliingia fainali hiyo baada ya kuongoza kundi A na kujihakikishia nafasi ya kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21. Timu hizo zilitakiwa kucheza mchezo wa fainali ili kupata mshindi wa Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2019/20.
Baada ya filimbi ya mwisho ya kumaliza mchezo kupulizwa uwanja mzima wa Chamazi ulirindima kwa kelele za furaha na matarumbeta kutoka kwa mashabiki wao waliosafiri na timu yao kutoka Dodoma kuja kuishangilia timu yao.
Baada ya mtanange huo kuisha, Mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe alikabidhi kikombe cha ubingwa kwa nahodha wa Dodoma Jiji FC Mbwana Kibacha mbele ya Rais wa TFF Wallace Karia na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa Leodger Tenga.
Baada ya Dodoma Jiji kutwaa ubingwa wa FDL kulikuwa na zawadi zingine kwa washindi mbalimbali, timu ya Iringa United imefanikiwa kutwaa zawadi ya Timu yenye nidhamu 2019/20, Jacob Masawe wa Gwambina FC amepata zawadi ya mchezaji bora wa FDL 2019/20, wakati zawadi ya golikipa bora imeenda kwa Andrew Kayuni wa Ihefu SC ya Mbeya, mfungaji bora imeenda kwa Anuary Jabir wa Dodoma Jiji FC na Kocha Bora wa mashindano imeenda kwa Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC Mbwana Makata.
Wachezaji wa Dodoma Jiji FC wakishangilia ushindi wao katika fainali ya FDL.
Mgeni rasmi wa mchezo wa fainali ya Ligi Daraja la Kwanza Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Godwin Gondwe (mwenye koti jeusi) baada ya kumkabidhi nahonda wa Dodoma Jiji FC Mbwana Kibacha kikombe cha ubingwa wa FDL.
Mshambuliaji wa Dodoma Jiji FC Anuary Jabir akiwa na zawadi ya kikombe cha mfungaji bora wa mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza FDL 2019/20.
Iringa United mshindi wa zawadi ya Timu yenye nidhamu
Andrew Kayuni golikipa wa timu ya Ihefu ndiye aliyechaguliwa kuwa golikipa bora wa mashindano.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.