NDUGU wawili Dodoma Jiji FC na Mbeya City FC zimegawana pointi moja moja baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana katika mchezo wa duru la sita la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mchezo uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Dodoma Jiji FC, Mbeya City na KMC ni timu ambazo ziko Ligi Kuu na zote zinamilikiwa na Halmashauri za maeneo yao. Huu ni mchezo wa kwanza Dodoma Jiji inakosa kupata ushindi katika uwanja wake wa nyumbani. Dodoma Jiji FC ilipata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Mwadui FC, ikaishinda JKT Tanzania 0-2 katika uwanja huo huo (ambapo yenyewe ilikuwa ugenini) na ikarejea kama mwenyeji kwenye mchezo na Ruvu JKT na kushinda bao 2-0.
Dodoma Jiji FC inafikisha jumla ya alama 11 ikishika nafasi ya 5 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikitanguliwa na vinara Azam FC (18), Simba SC (13), Yanga SC (13) na Biashara United FC (13).
Mbeya City FC wako nafasi ya 18 na alama zao 2 tu wakiwa wameshuka dimbani mara sita na kuambulia sare 2 (kwenye mchezo na Tanzania Prisons na leo dhidi ya Dodoma Jiji FC), na hawana goli hata moja.
Dodoma Jiji FC sasa watasafiri kwenda Kagera kwenye uwanja wa Kaitaba Bukoba kupambana na timu nyingine kongwe ya Ligi Kuu inayosuasua 'wakata miwa' wa Kagera Sugar Oktoba 20.
Katika mchezo wa leo Dodoma Jiji FC iliwakilishwa na Aron Kalambo, George Wawa, Abubakari Ngalema, Mbwana Kibacha (Nahodha), Augustino Samson, Rajab Mgalula, Dickson Ambundo, Cleophace Mkandala, Anuary Jabiri, Khamis Mcha na Jamal Mtegeta, na wachezaji wa akiba walikuwa Emmanuel Mseja, Anderson Solomon, Hassan Kapona, Steven Mganga, Omary Kanyoro, Santos Thomas na Peter Mapunda
Kila la heri Dodoma Jiji FC katika mchezo unaofuata. "Timu yetu, Jiji letu"
Manahodha wa Dodoma Jiji FC Mbwana Kibacha (jezi Namba 15) na Mpoki Mwakinyuke wa Mbeya CIty FC wakisalimiana kabla ya mchezo kati ya timu zao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.