LIGI ya mpira wa miguu Tanzania bara imeendelea leo Disemba 12 kwa michezo kadhaa ambapo timu inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dodoma Jiji FC imeshuka dimbani ikiikaribisha Gwambina FC kutokea Jijini Mwanza katika uwanja wa Jamhuri Jijini hapa na kuibuka kidedea kwa ushindi wa goli moja lililofungwa na mshambuliaji Seif Karihe dakika ya 45.
Akizungumza baada ya mchezo huo kocha wa Dodoma Jiji FC Mbwana Makata amekipongeza kikosi chake pamoja na benchi la ufundi kwa ushindi huo ambao umewapandisha kutoka nafasi ya 13 mpaka nafasi ya 8 katika msimamo wa ligi hiyo.
“Mchezo ulikuwa wa ushindani mkubwa hasa katika kipindi cha kwanza lakini tuliweza kutumia makosa waliyoyafanya wapinzani wetu na tukapata matokeo ambayo yametusogeza mpaka kwenye nafasi ya 8 ya msimamo wa ligi” Alisema Makata.
Makata aliongeza kuwa, kwa sasa nguvu zote wanazihamishia kwenye mchezo unaofuata ambao watasafiri hadi Jijini Arusha kuikabili timu ya wananchi Yanga mchezo unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ya tarehe 19 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta Jijini humo.
Kwa upande wake Kocha wa Gwambina FC Fulgence Novatus alisema kuwa, mpira wa miguu ni mchezo wa makosa na Dodoma Jiji FC wameyatumia makosa hayo kuwaadhibu na kupelekea wao kupoteza mchezo huo.
“Tulipata nafasi nyingi lakini hatukuzitumia na kama unavyojua soka ni mchezo wa makosa ukifanya makosa kidogo mwenzako anaweza kuyatumia kukuadhibu, tumepoteza lakini ligi bado inaendelea na tunahamishia nguvu katika mchezo wetu unaofuata.” Aliongeza Novatus.
Picha za baadhi ya matukio:
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.