TIMU ya mpira wa miguu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dodoma Jiji FC imepoteza mchezo mwingine ikiwa ugenini kwa kufungwa magoli 3 - 1 leo iliposhuka dimbani kukabiliana na vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Yanga ambao ndiyo walikuwa wenyeji katika mchezo uliochezwa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta Jijini Arusha.
Dodoma ndiyo walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia kwa mshambuliaji Seif Abdallah Rashid Karihe mnamo dakika ya tatu tu ya mchezo akimalizia mpira uliotemwa na mlinda mlango wa Yanga SC Metacha Mnata, goli ambalo lilidumu kwa dakika 23 tu baada ya beki Lamine Moro kusawazisha kutokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Deus Kaseke.
Yanga walipata goli la pili kupitia kwa Saidi Ntibanzonkiza kwa mpira wa adhabu waliyoipata baada ya mshambuliaji huyo kuangushwa na Salmin Hoja nje kidogo ya eneo la kumi na nane, huku Bakari Mwamnyeto akiifungia Yanga goli la tatu kwenye dakika ya 75 na kufanya mchezo huo kumalizika kwa Dodoma Jiji kupoteza kwa magoli matatu kwa moja.
Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa Dodoma Jiji FC Mbwana Makata alisema licha ya kupoteza mchezo huo bado wanayo nafasi ya kufanya vizuri huku akiwapongeza wachezaji wake kwa ushindani waliouonesha dhidi ya Yanga na kwamba kwa sasa wanajipanga kwa mchezo wao unaofuata dhidi ya Mtibwa utakaochezwa Mkoani wa Morogoro Jumatano Disemba 23, 2020.
Kwa upande wake kocha mkuu wa Yanga Cedric Kaze alisema hawakutarajia ushindani walioupata kutoka kwa timu ya Dodoma na ameyaona mapungufu katika mchezo huo na yeye pamoja na benchi la ufundi watayafanyia kazi ili yasijitokeze katika mchezo unaofuata.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.