HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeendelea kufanya afua ya upuliziaji wa viuadudu vya kuangamiza viluwiluwi wa mbu waenezao ugonjwa wa Malaria kwa awamu ya tatu, zoezi lililoanza tarehe 28/09/2020 na kukamilika leo 02/2/2020.
Ikumbukwe kuwa tarehe 22 Juni, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli alizindua rasmi upuliziaji wa viuadudu katika maeneo yote nchini ili kutokomeza Mbu waenezao Malaria.
Aidha, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu aliwatangazia Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutekeleza zoezi la kuchukua viuadudu hivyo ili kupunguza kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria mara zoezi la utekelezaji litakapokamilika.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma hadi sasa imepokea jumla ya lita 21,360 ambapo lita20,480 zilipokelewa awamu ya kwanza mwaka 2017 na lita 880 zilipokelewa mwaka 2020 na zote kwa pamoja zimepulizwa katika maeneo mbalimbali ya mazalia ya Mbu katika Jiji la Dodoma.
Naye Afisa Afya wa Jiji la Dodoma Abdallah Mahia amewasisitiza wataalam kufanya upuliziaji wa viuadudu kwa kuzingatia miongozo na Wizara ya Afya kama inavyofanyika jijini hapa. Hii itawezesha kupata matokeo tarajiwa ya kutokomeza Mbu ili kudhibiti ugonjwa wa Malaria nchini.
Mahia amesema hadi sasa Kata zilizofikiwa na zoezi hili ni Miyuji, Ntyuka, Nzuguni, Nkuhungu, Madukani, Chamwino, Kiwanja cha Ndege, Mnadani, Msalato, Matumbulu, Hombolo, Ipagala, Hazina na Dodoma Makulu.
Vilevile, baadhi ya wananchi waishio Jijini Dodoma waliotakiwa kutoa maoni yao kuhusiana na zoezi hili wamemshukuru na kumpongeza kwa dhati Mhe. Dkt. John Magufuli kwa kutekeleza kwa vitendo mapambano dhidi ya Malaria nchini.
Anna Makali mkazi wa Kata ya Msalato alisema "kwa kweli tunamshukuru sana Rais wetu Magufuli kwa kusaidia hadi Serikali imetoa madawa haya ya kuua mazalia ya Mbu kwenye mitaa yetu. Kwa kweli mimi binafsi na watu wote hapa tunampongeza sana"
Aidha, wamemshukuru Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru na Halmashauri ya Jiji hili kwa jitihada zinazochukuliwa na Jiji hili kutekeleza zoezi hili muhimu.
Afisa Afya wa Jiji la Dodoma Abdallah Mahia alipokuwa akielezea juu ya zoezi la upuliziaji wa viuadudu vya kuangamiza viluwiluwi wa mbu waenezao ugonjwa wa Malaria Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.