TIMU ya Dodoma Jiji FC imeendelea kujinoa na mazoezi makali kuelekea kukabiliana na timu ya Njombe Mji FC ya Mkoani Njombe katika mchezo wa ligi daraja la kwanza Tanzania Bara utakaochukua nafasi katika dimba la CCM Jamhuri Jijini Dodoma Jumamosi hii Machi 14, 2020 kuanzia saa kumi kamili jioni.
Mahojiano maalum ya awali na msemaji wa timu hiyo, Ramadhani Juma alisema kuwa, kwa sasa wanaongoza kundi A kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa dhidi ya Ihefu SC ya Mbarali Mbeya huku timu zote zikiwa na pointi 36.
Juma alisema kikosi chake kinaendelea na mazoezi ili kuwa imara zaidi kuelekea kumkabili mpinzani wao ambaye anashikilia nafasi ya tano akiwa amecheza mechi 17 akiwa na alama 26, tofauti ya alama 10 huku Dodoma Jiji FC ambao wanaongoza ligi daraja la kwanza kundi A ikiwa na alama 36.
“Dodoma Jiji FC kwa msimamo wa ligi kwa sasa tuko katika nafasi nzuri, hatujaridhika bado tunaendelea kupambana ili tujiweke katika nafasi nzuri zaidi ya kupanda ligi kuu msimu ujao, kila mechi kwetu tunaicheza kama fainali ukizingatia mechi mbili mfululizo tumepata ushindi.
“Tumejiandaa vizuri mechi kwa inayokuja dhidi ya Njombe Mji FC, kwa sababu tumewazidi alama 10 kila timu inang’ang’ana kuwa na alama nzuri zaidi kwa hiyo tunajua ugumu wa mechi ndiyo maana kocha anafanyia kazi makosa yaliyopita na kutengeneze ‘game plan’ kwa ajili ya mechi ijayo,” alisema Juma.
Kwa upande wake Kocha wa timu ya hiyo, Mbwana Makata alitoa wito kwa mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi ili kutoa hamasa kwa vijana hao ili wazidi kufanya vizuri zaidi.
“Kikubwa tu mashabiki wetu nawapongeza sana kwa kuendelea kuwa bega kwa bega na sisi na niwaombe tu tuendelee kuisapoti timu yetu, na nina imani Jamhuri tutakuwa wote niwaahidi tu hatutawaangusha”, alisema Makata.
Timu ya Dodoma Jiji FC ipo kileleni mwa kundi A ikiwa na alama 36 ikifuatiwa na Ihefu, Mbeya Kwanza, Majimaji FC, Njombe Mji FC, Friends Rangers, African Lyon, Boma FC, Cosmopolitan, Pan African, Iringa United na Mlale FC ambao wanaburuza mkia katika kundi hilo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.