TIMU ya Dodoma Jiji FC inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma leo imetimiza azma yake ya kupanda Ligi Kuu ya Vodacom msimu ujao baada ya kushinda mchezo wake dhidi ya Iringa United kwa ushindi wa mabao 2 - 0 kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma leo Jula 11, 2020.
Mchezo huo ni wa mwisho kwa Ligi Daraja la kwanza msimu huu ambapo vinara hao wa kundi A wamekuwa washindi wa kundi na kuungana na Gwambina FC ya Misungwi Mwanza kupanda daraja moja kwa moja.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin alisema watahakikisha wanafanya usajili kwa umakini mkubwa na kuiandaa timu vizuri ili kuhakikisha wanafanya vizuri kunako Ligi Kuu ya soka Tanznaia Bara inayotarajiwa kuanza mwezi ujao, huku akizitahadharisha timu kubwa za Simba na Yanga kuwa zijiandae kupokea vipigo katika michezo watakayokutana na timu hiyo.
"Simba wakija hapa ni kipigo na Yanga wakija hapa ni kipigo tu, tutaiandaa timu kuwa ya ushindani mkubwa kwa kufanya usajili mzuri na kuwa na kambi nzuri" alisema Kunambi.
Kwa mujibu wa Msemaji wa timu hiyo Ramadhani Juma, Dodoma Jiji FC sasa inajiandaa kucheza fainali ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Gwambina katika mchezo wa kusaka heshima utakaopigwa kwenye dimba la Azam Complex Chamazi Jijini Dar es Salaam Jumamosi ya Julai 18 mwaka huu.
Juma alisema baada ya mchezo huo, timu itarejea kambini Dodoma kwa ajili ya taratibu za kuvunja kambi kwa muda kabla ya kurejea tena na kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2020/2021.
"Kwanza tunamshukuru Mungu aliyetuwezesha kufikia lengo kuu la timu yetu na la kila mkazi wa Dodoma ambalo ni kupanda Ligi Kuu, lakini pili tunawshukuru wadau wote kwa ushirikiano walitoa kwa uongozi na timu kwa ujumla, Waandishi wa Habari na mashabiki wetu pamoja na wadau wengine wote wamefanya kazi kubwa sana kwa ajili ya timu yao, na mwisho wa siku wamevuna walichokipanda na sasa wanasubiri uhondo wa Ligi Kuu wakiwa na timu yao ya nyumbani kabisa" alisema.
Aidha, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kupitia ukurasa wake rasmi wa instagram imeipongeza Dodoma Jiji FC na kuikaribisha katika ligi hiyo inayoisimamia.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.