KLABU ya soka ya Dodoma Jiji imeibuka na ushindi ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani siku ya jumapili kwa kuichapa timu ya Tanzania Prison magoli mawili kwa moja huku mechi hiyo ikichezwa usiku kwa mara ya kwanza katika historia ya soka Mkoani Dodoma na Tanzania bara nje ya Dar es Salaam.
Prison wao walianza kupata goli la mapema katika dakika ya tatu na baadae Walima Zabibu kurudi mchezoni na kusawazisha kupitia kwa Khamis Mcha aliyefunga kwa mkwaju wa penati mnamo dakika ya 31 ya mchezo huku goli la ushindi likifungwa na Emmanuel Martin katika dakika ya 59 akipokea pasi safi kutoka kwa Abubakar Ngalema.
Akizungumza baada ya mchezo kumalizika Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji Mbwana Makata amesema kuwa ilikua ni mechi muhimu sana kwao kwani hawakua katika nafasi nzuri hivyo walitakiwa washinde ili kujiweka katika tatu bora ndani ya msimamo wa ligi kuu ya NBC Tanzania Bara.
Makata pia amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kuonesha soka safi licha ya wapinzani kucheza mpira mzuri na kupata goli la mapema bado walipambana na kuwa bora zaidi na kupelekea kuondoka na alama tatu muhimu nyumbani.
“Ulikua ni mchezo mzuri wenye ushindani, wenzetu walipata goli la mapema katika dakika ya tatu ila wachezaji wangu hawakutoka mchezoni walipambana tukasawazisha na kupata goli la ushindi” alisema Makata.
Katika hatua nyingine Afisa Habari wa timu hiyo Moses Mpunga ameipongeza TFF, Bodi ya ligi na Azam kwa kuweka taa katika dimba hilo kwani imesadia kuongeza mshabiki ambao hapo awali walikua wakikosa fursa ya kuja uwanjani kutokana na kuwa katika shuguli zao muda ambao mechi zilikua zikichezwa.
Mpunga ameongeza kuwa hatua hiyo itapelekea mechi nyingi kuchezwa usiku jambo ambalo licha ya kupata mashabiki wengi na kuongeza mapato pia itaisaidia timu hiyo kucheza mpira katika muda mzuri ambao hautakua na jua kitu kinachoweza kupelekea matokeo mazuri kwa timu hiyo.
“Mchezo umemalizika na kwa sasa macho yetu tumeyaelekeza katika mchezo wetu dhidi ya Mtibwa ambapo tutakua ugenini ni mchezo mgumu lakini tunaamini tutashinda kutokana na mikakati tuliyojiwekea” alisema Mpunga.
Dodoma Jiji imepanda kutoka nafasi ya kumi mpaka nafasi ya tatu ikiwa na alama saba huku tayari ikiwa imeshacheza michezo minne.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.