TIMU ya Mpira wa Miguu ya Dodoma Jiji inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara imewasili salama Mkoani Pwani kuwakabili Ruvu Shooting siku ya Jumatano tar. 05.03.2021 saa 10:00 jioni katika dimba la Mabatini.
Kikosi hicho chenye wachezaji 20, benchi la ufundi pamoja na viongozi kiliondoka Jijini Dodoma alfajiri siku ya jana na kuwasili Pwani majira ya saa 7:30 mchana na kikafanya mazoezi katika uwanja wa Karume Kongowe majira ya saa kumi jioni.
Dodoma Jiji FC ipo Mkoani Pwani kusaka alama tatu muhimu huku ikiwa na rekodi nzuri katika mchezo uliopita dhidi ya Ruvu mchezo ambao ulimalizika kwa Dodoma Jiji kuondoka na alama tatu ikishinda 2 – 0.
Walima Zabibu wanahitaji kushinda mchezo huo unaoonekana kuwa na ushindani mkubwa ili kujihakikishia nafasi katika tano bora ya Ligi hiyo.
Akizungumza na Mwandishi wetu Afisa Habari wa Dodoma Jiji FC, Moses Mpunga amesema kuwa wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo na kuwa watacheza kwa nidhamu kubwa kwani Ruvu Shooting ni timu nzuri na yenye uzoefu na Ligi lakini hilo halitawazuia wao kuondoka na alama tatu.
“Tutaingia kwa tahadhali kubwa tukiamini tunacheza na timu nzuri na yenye uzoefu lakini ukiangalia ubora wa timu iko wazi kuwa kikosi chetu ni bora kuliko chao hivyo uzoefu wao hautatuzuia sisi kuondoka na alama tatu katika uwanja wao wa nyumbani”Alisema Mpunga.
Aidha Dodoma Jiji FC itacheza mechi mbili za ugenini ambapo baada ya Ruvu Shooting itasafiri kuelekea Jijini Mbeya kuwakabili Mbeya City siku ya Jumatatu Machi nane.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.