KATIKA kuhakikisha wanaunga mkono kauli mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu inayosema “Kazi iendelee” kikosi cha Dodoma Jiji kimerejea jana usiku kutokea Mkoani Rukwa na bila kupumzika leo kimefanya mazoezi ya viungo kujiandaa na mchezo wao dhidi ya klabu ya Namungo siku ya tarehe 18/04/2021.
Dodoma Jiji itakua mwenyeji kwenye mchezo huo utakaochezwa katika dimba la Jamhuri almaarufu kama Machinjioni kuanzia saa 10:00 jioni.
Meneja wa timu hiyo Mwl. Onesmo Lubeleje amesema kuwa hawana muda wa kupoteza kupumzika wakati wana mchezo muhimu kwao ambao wakishinda utawafanya wazidi kujichimbia kunako tano bora ya ligi Kuu Tanzania Bara.
Mwl. Lubeleje amesema kuwa licha ya kuwa nyumbani katika mchezo huo, wanajua kuwa Namungo ni timu nzuri ambayo wasipojiandaa wanaweza kupata matokeo mabaya hivyo ni lazima wajiandae kuwakabili ili waweze kupata matokeo ukizingatia katika mchezo wao uliopita walipoteza kwa kufungwa goli moja wakiwa ugenini.
“Namungo ni timu nzuri ndio maana inashiriki kombe la Shirikisho Barani Africa ila hilo halitutishi kutokana na ubora wa kikosi chetu hivyo hatujaona haja ya kupumzika tumeanza mazoezi rasmi na niwatoe hofu mashabiki wetu kuwa tunaenda kupata matokeo mazuri katika mchezo huo” alisema Mwl. Lubeleje.
Akizungumzia hali ya wachezaji mmoja mmoja Daktari wa timu hiyo Dkt. Juma Kiswagala amesema kuwa Salmini Hoza alipata matatizo ya misuli pamoja na Anuary Jabir ambaye aliumia mguu katika mechi dhidi ya Prisons ila wote hali zao zinaendelea vizuri na leo walijiunga na wachezaji wenzao katika mazoezi hivyo wote watacheza katika mchezo dhidi ya Namungo kama Kocha atahitaji huduma yao.
Sasa Dodoma Jiji wamefikisha alama 37 wakiwa katika nafasi ya tano baada ya kucheza michezo 25.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.