HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeingia makubaliano ya utunzaji na upambaji wa maeneo ya barabara yenye mizunguko (round about) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA), ambapo Mamlaka hiyo itahudumia maeneo hayo kwa kutunza bustani za maua na kuweka sanamu za wanyama ikiwemo Tembo.
Hafla ya kusaini hati ya makubaliano imefanyika leo Julai 2, 2018, katika Ukumbi mdogo wa Mikutano wa Jiji la Dodoma na kuhudhuriwa na Mstahiki Meya wa Jiji hilo Profesa Davis Mwamfupe na Mkurugenzi wa Jiji Godwin Kunambi, huku Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ikiwakilishwa na Ofisa Uhusiano Mkuu wa Mamlaka hiyo Joyce Mgaya kwa niaba ya Mhifadhi.
PICHA: Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kulia) akimkabidhi hati ya makubaliano Ofisa Uhusiano Mkuu wa Mamlaka ya Uhifadhi ya Ngorongoro Joyce Mgaya kwa niaba ya Mhifadhi, mara baada ya kutiliana saini makubaliano ya kuboresha Mazingira ya Mji wa Dodoma na kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo Nchini.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali, Mkurugenzi Kunambi alisema wamekubaliana kuwa, maeneo matatu ya mizunguko yatakabidhiwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, ambapo moja lipo barabara ya Dodoma-Dar es Salaam eneo la Ipagala, jingine lipo barabara ya Dodoma-Singida, na eneo la tatu ni mzunguko uliopo barabara ya Dodoma-Babati jirani na uwanja wa ndege.
PICHA: Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka Ngumu Dickson Kimaro akifafanua baadhi ya mambo kwa Waandishi wa Habari wakati wa makabidhiano ya maeneo ya mizunguko ya barabara katika Mji wa Dodoma yatakayoboreshwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambapo pia yatatumika kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo Nchini.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Joyce Mgaya alisema baada ya kukabidhiwa maeneo hayo na Jiji la Dodoma, Mamlaka itaanza mara moja kazi ya kuyaboresha na kuweka sanamu za baadhi ya wanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo ili kuufanya Mji wa Dodoma kuvutia zaidi na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Nchini.
Kwa upande wake, Mstaki Meya Profesa Mwamfupe alisema Mji wa Dodoma unahitaji juhudi za Jiji na wadau mbalimbali kuupendezesha kwa kuzingatia kuwa ndiyo Makao Makuu ya Nchi, huku akitoa wito kwa wakazi wa Jiji hilo kudumisha usafi wa mazingira kwenye makazi yao na maeneo ya biashara ili Mitaa yote ya Mji wa Dodoma iwe safi muda wote.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.