TIMU ya Dodoma Jiji FC kwa mara ya kwanza leo tarehe 24 Oktoba, 2021 katika dimba la nyumbani uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma inashuka kucheza usiku dhidi ya Tanzania Prisons kutoka Jijini Mbeya.
Huu ni mchezo wa kwanza kwenye historia ya Ligi Kuu Tanzania bara kuchezwa usiku nje ya Jiji la Dar es Salaam. Mchezo huo utaanza sasa 1 usiku na kiingilio ni shilingi 5,000 katika Jukwaa Kuu na shilingi 3,000 jukwaa la mzunguko.
Dodoma Jiji FC inaingia katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare tasa katika mchezo wake uliopita dhidi ya Mbeya Kwanza ambao Dodoma Jiji ilikuwa ugenini. Ilihali Tanzania Prisons SC ilitoka sare tasa ugenini pia dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Katika ukurasa rasmi wa instagram, Prison wameandika kuwa “Mchezo utakuwa mgumu kutokana na maandalizi ya timu zote mbili ila ni muhimu sana kwetu kwani tunahitaji kupata alama tatu (3).”
Hata hivyo Prison wamekiri kuwa “Licha ya uzuri wa timu ya Dodoma Jiji katika michezo yao ya hivi karibuni, kama timu tumejipanga na tupo tayari kukabiliana nao.” Wamesema Prison kwa tahadhari.
Dodoma Jiji inataka kuweka historia kwa kushinda mchezo huu wa kwanza kuchezwa usiku kwenye uwanja wao wa nyumbani baada ya kucheza mechi kadhaa usiku Jijini Dar es Salaam.
Akiongea na tovuti hii, mmoja wa viongozi wa Dodoma Jiji FC, Fredy Mwakisambwe amesema "Ni mchezo muhimu sana kwetu, tunashukuru timu iko vizuri na imefanya mazoezi ya kutosha kujiandaa na mchezo huu, uongozi umeshafanya majukumu yake na sasa ni jukumu la benchi la ufundi na wachezaji kukamilisha sehemu yao na kuwapa furaha wananchi wa Dodoma" amesema Mwakisambwe kwa kujiamini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.