Ili kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato kwa mwaka 2020/2021 Jiji la Dodoma limebainisha njia saba za ukusanyaji mapato ikiwemo kuwatumia watendaji wa kata na mitaa ili waweze kukusanya mapato katika maeneo yao.
Njia nyingine ni pamoja na kufanya uchambuzi wa vyanzo vya mapato vya halmashauri ili kukusanya takwimu sahihi za vyanzo hivyo, kuhakikisha ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo na vituo vyote unatumia vifaa na mfumo wa kielektroniki ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Akizungumza katika baraza la madiwani wakati wa uwasilishaji mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amesema mkakati mwingine ni kuboresha minada ya Mpunguzi, Kikombo na Hombolo.
Aidha, amesema watakua wanaandaa 'database' ya viwanja vyote vinavyozalishwa ili kudhibiti utoaji/ulipaji na uendelezaji, kuandaa mfumo wa ufuatiliaji wa majalada yote ya halmashauri ikiwemo yanayohusu mapato pamoja na kufanya tathimini ya madeni ambayo halmashauri inadai ili kuongeza mapato.
Mikakati hiyo imekuja baada ya mapato ya Jiji hilo lilikoshika namba mbili kwa ukusanyaji wa mapato huku likiongoza kwa mapato ghafi kupungua kutoka kukusanya Sh Bilioni 177 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hadi Sh Bilioni 116 kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Kunambi amesema kwa mwaka huu wa fedha Jiji la Dodoma limekadiriwa kukusanya mapato jumla ya Sh Bilioni 116 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani (own source), Serikali Kuu na wahisani mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo, utoaji huduma na kujiendesha.
Amesema sababu za kupungua huko kwa mapato kumetokana na kupungua kwa vyanzo vya mapato ya nje na ya ndani. Vyanzo vya mapato ya nje ni ruzuku toka serikali Kuu na kutoletewa fedha toka kwa wahisani kwa miradi ya TSCP, TASAF, SEDEP na EQUIP.
"Mapato ya ndani yamepungua kutokana na kupungua kwa mapato yanayotokana na Idara ya Ardhi, Mipangomiji na Maliasili ambapo kwa mwaka wa fedha ulioisha walikadiriwa kukusanya asilimia 30 ya bajeti yote lakini kwa mwaka huu wa fedha imekusanya asilimia 26 ya bajeti yote.
Lakini sasa tunaamini kwa mikakati tuliyojiwekea tunaenda kufanya vizuri tena kwenye ukusanyaji, tumejipanga kuhakikisha hakuna mapato yatakayopotea," Amesema Kunambi.
Katika kikao hicho cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma alifafanua kwa undani utekelezaji wa miradi maendeleo na utoaji huduma katika jiji la Dodoma kwa kipindi cha hadi kufikia Disemba, 2019 ikiwa ni utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi akifanya wasilisho la utekelezaji wa miradi na utoaji huduma kwa kipindi cha hadi Disemba, 2019 wakati wa kikao cha baraza la madiwani wa Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.