Kikosi cha Dodoma Jiji leo kimefanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya kuikabili Simba SC katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (AFSC) utakaochezwa katika dimba hilo kesho Jumatano ya tarehe 26/05/2021 saa moja kamili usiku.
Dodoma Jiji yenye maskani yake katikati ya nchi yalipo Makao Makuu ya Serikali Dodoma, inakutana na Simba kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo, ikiwa na rekodi ya kutopoteza mchezo hata mmoja huku ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya magoli kuliko timu yoyote ndani ya ligi hiyo ndani ya msimu huu.
Walima zabibu hao wana jumla ya magoli 14 ya kufunga kati ya michezo mitatu waliyocheza kwenye FA msimu huu, ambayo ni Dodoma Jiji 5 – 1 Hollywoof FC, Dodoma Jiji 7 – 0 Kipigwe FC na Dodoma Jiji 2 – 0 KMC.
Licha ya burudani muruwa inayotokana na mpira mzuri wanaoucheza Dodoma Jiji, timu hiyo imekua tishio kwa vilabu vingi kutokana na kupata matokeo katika viwanja vigumu nchini, hivyo kuufanya mchezo wake dhidi ya Simba kuwa na mvuto mkuwa kwa mashabiki na wapenzi wa soka kutokana na timu hizo kucheza mchezo unaoshabihiana.
“Mechi hii ni muhimu kwenu kwani itaangaliwa na watu wengi hivyo nenda kaoneshe uwezo wako mwisho wa siku italeta mafanikio kwa mtu mmoja mmoja na timu kwa ujumla” hiyo ni moja kati ya kauli ilizoziongea Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji Mbwana Makata kwa wachezaji wake baada ya mazoezi ya mwisho leo.
Dodoma Jiji inawakosa nyota wake wawili ambao ni Anuary Jabir na Rajab Mgalula walikua nje ya kikosi kutokana na kuwa majeruhi.
Kila la heri Timu yetu, Jiji letu
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.