KIKOSI cha Dodoma Jiji FC kimetoshana nguvu na timu ya Mbeya City baada ya kutoka sare ya 1 – 1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana katika dimba la Sokoine Jijini Mbeya.
Dodoma Jiji FC ndio waliokua wa kwanza kupata goli katika dakika ya 22 ya mchezo kupitia kwa Seif Karihe aliyepokea pasi kutoka kwa Dickson Ambundo, huku goli la kusawazisha la Mbeya City likifungwa na Juma Liuzio mnamo dakika ya 59 magoli yaliyodumu hadi kumalizika kwa mchezo huo.
Akizungumza baada ya mchezo huo Meneja wa Dodoma Jiji FC Onesmo Lubeleje amesema kuwa mchezo huo ulikua mgumu kutokana na nafasi ya Mbeya City katika msimamo wa ligi hivyo wanashukuru hata kwa matokeo hayo kwani kupata pointi moja ugenini sio matokeo mabaya sana.
“Mbeya City ni timu nzuri ila tu walikua wamekosa matokeo na ukizingatia wapo chini kabisa katika msimamo wa ligi Kuu jambo lililopelekea mechi hiyo kuwa ngumu kwa upande wetu, ila tunashukuru wachezaji wetu wamepambana na kupata angalau pointi moja ugenini” Alisema Lubeleje.
Lubeleje aliongeza kuwa kwa sasa wanahamishia nguvu katika mchezo wao unaofuata dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma siku ya Ijumaa tarehe 12.03.2021 saa 10:00 jioni.
Aidha matokeo hayo ya Dodoma Jiji FC yanaipandisha timu hiyo kwa nafasi moja hadi nafasi ya 6 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imecheza michezo 23 na kujikusanyia alama 33.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.