HISTORIA mpya inatarajiwa kuandikwa kesho tarehe 5.11.2020 kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma kushuhudia sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza tangu kupata Uhuru.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge katika mkutano wake na waandishi wa habari Jijini Dodoma, alipokua akizungumzia kuhusu maandalizi ya sherehe hizo ambazo wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla watashuhudia kuapishwa kwa Rais mteule Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa Jamhuri Jijini hapa.
Dkt. Mahenge amesema kuwa ni heshima kubwa kwa Mkoa wa Dodoma kupata fursa ya kushuhudia tukio hilo la kistoria ambalo hufanyika mara moja ndani ya miaka mitano na anaamini kuwa limeleta mianya ya biashara na kuinua uchumi ndani ya Mkoa wa Dodoma.
“Haya ni matunda makubwa ya uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Mkoani Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa ndoto ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyoanza kuitekeleza mwaka 1973”, Alisema Dkt. Mahenge.
Amesema kuwa matukio makubwa kama haya yatakuwa yakifanyika Mkoani Dodoma na kutoa fursa na hamasa kwa wawekezaji kama vile wa huduma za usafiri, mahoteli, nyumba za kulala wageni, kumbi za burudani, mama lishe, machinga na wengine wengi.
Hata hivyo Dkt. Mahenge ametoa rai kwa wanachi wa Dodoma kutokua sehemu ya bugudha na usumbufu kwa wageni wanaokuja licha ya kuwa Dodoma ni sehemu yenye amani wakati wote hivyo amewataka kuimarisha na kudumisha sifa hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha viwango vya huduma na biashara zao.
“Sherehe hizi zitahudhuliwa na Marais na viongozi wa juu kutoka mataifa mbalimbali, viongozi wastaafu na wafanyabisha wakubwa hivyo tukiboresha huduma katika biashara zetu tutawavutia kurudi tena hata baada ya zoezi hili kuisha kwa ajili ya kutembea na kufanya uwekezaji mbalimbali” Aliongeza Dkt. Mahenge.
Aidha Dkt. Mahenge amesema kuwa sherehe hizo zitapambwa kwa burudani mbalimbali ikiwa ni pamoja na gwaride maalum lililoandaliwa na vikosi mbalimbali vya ulinzi vya Tanzania, vikundi vya ngoma, Pamoja na wasanii wa kizazi kipya kama vile Halmonize, Zuchu, Nandy, Sholo Mwamba na Dulla Makabila.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amewakaribisha na kuwahimiza wananchi wote kuwahi kufika uwanjani mapema ili kuepuka usumbufu na kuongeza kuwa milango itakua wazi kuanzia saa 12 alfajiri.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.