Na. Theresia Francis, Dodoma
Benki ya NMB imekabidhi vifaa vya kuhifadhia taka kwa Halmashaurim ya Jiji la Dodoma, kwa ajili ya kuhakikisha wakazi wake wanapata sehemu ya kuhifadhia taka na jiji linakuwa safi.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo jijini Dodoma katika uwanja wa Nyerere Square, ambapo Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori alikabidhi vifaa hivyo vya kuhifadhia taka 100 vyenye thamani ya shilingi milioni 20 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
“Tunajua jitihada zako kwenye suala zima la mazingira una dira kubwa ya kuonesha kwamba unahitaji Dodoma iwe ya kijani, tunakuahidi tutaendelea kuwa pamoja na wewe kuhakikisha Dodoma inakuwa ya kijani kupitia programu yetu ya kuwekeza kwa jamii. Sisi NMB tunafarijika sana kuona yanayotokea kwenye Jiji la Dodoma, naomba nichukue fursa hii kukupongeza kwa dhati kabisa kwa jitihada unazozichukua katika kuboresha mazingira ya Dodoma. Tunatambua kazi zote unazofanya na timu yako kwa kuhakikisha Dodoma inakua jiji linalovutia katika usafi” alisema Kimori.
Aidha, Kimori alisema kuwa NMB wanatambua hitaji la vifaa vya kuhifadhia taka kwa Jiji la Dodoma. Aliongeza kuwa benki yake inayatambua mahitaji ya jamii na watahakikisha wanatoa vifaa hivyo Dodoma kulingana na idadi inayohitajika.
Kimori alisema “...nikuhakikishie kwamba tunajua hitaji lako ni vifaa vya kuhifadhia taka 350 kwa jiji hili, leo tunakabidhi vifaa 100 tutaendelea kushirikiana na wewe kuhakikisha idadi inatimia. Benki ya NMB inajua umuhimu wa jamii na kila mwaka tunatenga zaidi ya bilioni mbili kupeleka kwenye jamii katika maeneo mbalimbali kama afya, elimu, mazingira na kutoa elimu ya fedha kwa jamii yetu, mazingira ni moja ya nguzo ambazo tunaziangalia na mkoa wa Dodoma mnaonyesha mfano kwa jinsi ambavyo mnahimiza utunzaji wa mazingira.
Kimori alimalizia kwa kuwahimiza wana Dodoma kutunza vifaa walivyopewa viweze kudumu kwa muda mrefu, na kutumia kwa usahihi vifaa walivyopewa ili kutimiza lengo la mkuu wa mkoa na timu yake nzima kuhakikisha wana Dodoma hawatupi taka hovyo na mji unakua msafi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.