Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI wa Dodoma wametakiwa kuwa na utamaduni kuheshimu na kutunza usafi wa mazingira ili kulifanya Jiji la Dodoma kuwa safi na la kisasa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka katika hafla fupi ya ugawaji vifaa vya kuhifadhi taka katika bustani ya Nyerere square jijini Dodoma.
Mtaka alisema kuwa wananchi wa Dodoma lazima wawe na utamaduni wa kupenda usafi. “Namna bora ya kuwasaidia ni kwenda kwenye adhabu. Naibu Meya upo hapa, tuharakishe mchakato wa sheria ndogo zinazohusiana na usafi wa mazingira” alisema Mtaka.
Aliwataka wananchi kuacha tabia ya kutupa taka ovyo. Alisema kuwa mitaro mingi ni michafu katika Halmashauri ya Jiji. Aliagiza mitaro hiyo kusafishwa ili iweze kutumu na kufanya kazi iliyokusudiwa.
Aidha, alikemea tabia ya viwanja kutekelezwa bila kufanyiwa usafi. “Dodoma hatuhitaji viwanja pori, vinafuga wezi. Fyeka majani kwenye kiwanja chako na panda miti” alisema Mtaka.
Kwa upande wa Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Juma Kimori alisema kuwa benki yake itaendelea kuunga mkono juhudi za Mkoa wa Dodoma za kuboresha usafi wa mazingira. “Napenda kukupongeza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa juhudi zako za kuboresha mazingira ya Jiji la Dodoma ili livutie kwa usafi. Benki ya NMB tutakuwa nawe ili Dodoma iwe ya kijani” alisema Kimori.
Akiongelea zoezi la ugawaji wa vifaa vya kuhifadhia taka, alisema kuwa benki yake inatambua hitaji la vifaa vya kuhifadhia taka katika Jiji la Dodoma. Alisema kuwa idadi inayotakiwa ni vifaa 350 na kuahidi kuendelea kuunga mkono upatikanaji wake. “Rai yangu, tutumie na kutunza vifaa hivi ili kuliweka Jiji la Dodoma safi” alisema Kimori.
Kwa upande wa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Emmanuel Chibago alisema kuwa vifaa hivyo ni muhimu kwa halmashauri. “NMB mmetusaidia Halmashauri ya Jiji la Dodoma kupunguza mzigo katika bajeti yetu. Tutavitunza vifaa hivi ili viwe endelevu” alisema Chibago.
Benki ya NMB ilikabidhi vifaa 100 vya kuhifadhia taka katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma vyenye thamani ya shilingi milioni 20 kwa lengo la kurahisisha zoezi la kuhifadhi taka katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.